Marekani yatumia jeshi, diplomasia kudhibiti mgogoro wa Mashariki ya Kati

  • VOA News

Manuari ya jeshi la Marekani USS Dwight D. Eisenhower ikiwa iko katika Ghuba ya Uajemi, huko Mashariki ya Kati.

Huku ikionyesha nguvu za kijeshi na msukumo mkubwa wa suluhisho la kidiplomasia, Marekani inajaribu kudhibiti vita vipana huko Mashariki ya Kati.

Pamoja na historia ya vita vya Israel dhidi ya Hamas, majeshi yanayoungwa mkono na Iran katika eneo hilo yana nia ya dhati kuendeleza mashambulizi dhidi ya maslahi ya Magharibi.

Hata baada ya ushirika unaoongozwa na Marekani kufanikiwa kuyapiga malengo 36 ya Wahouthi nchini Yemen siku ya Jumamosi, Marekani haiwezi kufuta uwezekano wa mashambulizi zaidi yatakayofanya na Wahouthi au wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran huko Mashariki ya Kati, ameonye mshauri wa usalama wa taifa Jake Sullivan katika kituo cha televisheni cha ABC katika kipindi cha ‘This Week.’

Jake Sullivan

Jake Sullivan, Mshauri wa Usalama wa Taifa anaeleza kuwa: “Lengo kuu la mashambulizi limekuwa ni kuwaondolea uwezo wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran huko nchini Iraw na Syria ambao wameshambulia majeshi yetu kutoka kwa Wahouthi ambao wanaendelea kutishia meli kwenye Bahari ya Sham, na sisi tunaamini kuwa yamekuwa na matokeo mazuri ya kupunguza uwezo wa wanamgambo na wa Houthi. Kama ilivyo muhimu, tutaendelea kuchukua hatua.”

Lakini Wahouthi wameapa kuendelea na operesheni zao za kijeshi, ambazo wamethibitisha kuwa ni kulipiza kisasi kwa vita vya Israel dhidi ya malengo ya Hamas huko Gaza.

Zaidi ya Wapalestina 27,000 wamejikuta katikati ya mapigano na kuuawa na zaidi ya 66,000 wamejeruhiwa, kwa mujibu wa Wizara ya Afya inayoendeshwa na Hamas huko Gaza.

Shambulizi la mabomu lililofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza Jumamosi Disemba 16, 2023.

Nabil Mohsen Abu Nashtan, Waziri wa Nchi wa Yemen amesema: “Tunachokiona ni uchokozi, kuzingirwa, mauaji ya kimbari na kuzuia dawa kwenda kwa kaka zetu huko Gaza. Raia wa Yemen, makabila yake, silaha na wanaume wanajiweka tayari kukabiliana na uchokozi na kufanya kile ambacho wanaweza kukifanya.”

Kampeni za kijeshi za Israel zilianzishwa ikiwa ni majibu kwa uvamizi wa kigaidi wa Hamas ndani ya eneo la Israel hapo Oktoba 7. Takriban watu 1,200 waliuawa katika shambulizi na 240 zaidi walichukuliwa mateka. Siku ya Jumapili, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema vikosi 17 kati ya 24 vya Hamas vimeangushwa hadi hivi sasa.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel anasema: “Vikosi vingi vilivyobaki viko kusini mwa Ukanda wa Gaza na huko Rafah, na tutavishughulikia hivyo pia.”

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Marekani inaongezea msukumo wa suluhisho la kidiplomasia kwa mzozo huo huku kukiwa na ziara mpya ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken katika eneo hilo.

Pendekezo la hatua nyingi la kuongeza sitisho la mapigano na kuachiliwa kwa mateka kwa mabadilishano ya wafungwa wa kipalestina nchini Israel pia nalo linafanyikwa kazi.

Jake Sullivan, Mshauri wa Usalama wa Taifa anasema: “Rais ameweka nguvu yake katika hili. Amezungumza na viongozi kote huko Qatar na Misri, nchi mbili ambazo kwa hakika zimehusika katika kujaribu kupatikana kwa makubaliano, Sisi tuko katika mawasiliano ya mara kwa mara na wenzetu wa Israel katika hilo. Na Hamas inatakiwa nayo iwe tayari kusema ndiyo kwa mpango ambao utawarejesha nyumbani mateka.”

Sullivan alielezea kuwa makubaliano hayajakaribia kufikiwa na hakuna ratiba ambayo inaweza kutolewa.

Matamshi yake yamekuja baada ya Umoja wa Mataifa kuonya Ijumaa kwamba eneo la mpakani la Rafah, hasa, limekuwa nikinukuu “shinikizo baya la kukata tamaa” kwa Wapalestina wasiokuwa na makazi huko Gaza.

Ripoti ya Mwandishi wa VOA Verpnoca Balderas Iglesias.