Marekani yatahadharisha juu ya ukosefu wa usalama wa chakula Afrika

Dr. Cary Fowler

Maafisa wa Marekani wanasema ukosefu wa usalama wa chakula barani Afrika utakuwa mbaya zaidi mwaka huu kwasababu ya mabadiliko ya hali ya hewa, mizozo na kuvurugika kwa hali ya soko  kuliko sababishwa kwa kiasi na vita vya Russia nchini Ukraine.

Marekani inawasaidia wakulima wa Kiafrika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa kilimo cha umwagiliaji na hatua za kuvuna maji ili kuboresha uzalishaji chakula.

Akiongea na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao Alhamisi kutokea nchini Malawi, Cary Fowler, mwakilishi maalum wa Global Food Security, alisema wahusika wa mwaka 2022 kuhusu uhaba wa chakula barani Afrika wanaendelea.

Fowler anasema “natamani ningeweza kupeleka ujumbe wa matumaini kwamba mgogoro wa chakula utakwisha mwaka huu, lazima tutambue kwamba wahusika wakuu katika mgogoro wa chakula bado wako na sisi. Inatupasa sisi kuangalia masuluhisho yote hayo, au kuchukua hatua za kukabiliana nayo, hiyo ndiyo hali ambayo tunaiona leo.”

Mabadiliko ya Hali ya Hewa

Mabadiliko ya hali ya hewa, janga la ulimwengu, mizozo, na uvamizi wa Russia nchini Ukraine vyote vimelaumiwa kwa suala la ukosefu wa chakula na njaa barani Afrika.

Kwa mujibu wa ripoti ya 2022 ya Global Food Crisis, muafrika mmoja katika kila watano analala na njaa, na takriban watu milioni 140 katika bara hilo wanakabiliwa na ukosefu mkubwa sana wa chakula.

Wakulima wa kiafrika wanaendelea kutumia mbinu za kiasili za kilimo, lakini hali ya hewa isiyotabirika katika miaka ya karibuni, imesababisha wakulima kuzalisha chakula kidogo.

Wakulima wanalalamika kuhusu bei kubwa za mbegu na mbolea na kushindwa kuzalisha chakula cha kutosha kwa ajili ya watu.

Ukame pia umechangia ukosefu wa usalama wa chakula katika baadhi ya sehemu za bara hilo, hasa Pembe ya Afrika, umeharibu mifugo na mazao na kuwalazimsiha watu kutegemea misaada ya kibinadamu ya chakula na dawa.

Mwaka 2022, serikali ya Marekani iliwekeza dola bilioni 11 katika misaada ya kibinadamu kwenye nchi 55, ikiwemo baadhi kutoka Afrika.

USAID Global Food Crisis

Dina Esposito, Mratibu wa USAID Global Food Crisis, alisema serikali yake pia inawasaidia wakulima wa kiafrika katika kuzalisha chakula chao wenyewe ili kukabiliana na njaa na ukosefu wa chakula.

Esposito anasema “pia tuna mpango wa ulimwengu wa kukabiliana na njaa ambao kwa hakika unalenga kile ambacho kiko kwenye mifumo sahihi na mwelekeo wa kusukuma mbele kilimo, kuchukua hatua katika muktadha wa kieneo, kusukuma mbele juhudi za kilimo cha umwagiliaji na aina nyingine ya kuweka akiba ya maji ikiwa ni hatua za kuwasaidia wakulima kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa katika njia nyingine, kimsingi siku zote kuangalia—tunaona jukumu letu kwa kweli ni kuwasaidia wakulima kubadili mwenendo wa kilimo kwa kuzidisha na uzalishaji endelevu.”

Marekani Ina Nia ya Dhati

Esposito pia alisema serikali ya Marekani ina nia ya dhati kushirikiana na viongozi kusukuma mbele suala la uhaba wa chakula na kutatua tatizo la njaa ulimwenguni.

Koech Oscar anafundisha masuala ya ardhi, rasilimali za utawala na teknolojia ya kilimo katika chuo kikuu cha Nairobi. Anasema hakuna nchi hata moja ya kiafrika inaweza kutatua mgogoro wa chakula peke yake, kuna haja ya mwelekeo wa kikanda kukabiliana na ongezeko la njaa katika bara hilo.

Oscar anasema “tunahitaji mataifa yetu kufanya kazi pamoja kwasababu ya muingiliano uliopo. Mwisho wa siku tuna mfumo mmoja wa teknolojia, wanyama wetu wako Uganda. Baadhi yao wanakwenda nchini Tanzania na wengine wanakuja huku, kwahiyo tunahitaji mikakati ya kikanda kuzisaidia jamii zetu kwasababu haya ni matatizo ya kikanda na tunahitaji kuwekeza katika uzalishaji huu, hasa katika kilimo. Unaangalia bajeti za kitaifa katika nchi hizi za Kiafrika, kiasi kidogo kinakwenda katika kilimo kwasababu hatuwezi kuwa taifa lenye amani, hatuwezi kuwa taifa lenye ustawi, maendeleo, bila ya watu kuzalisha chakula chao wenyewe na cha kutosha kwa ajili yao.”

Oktoba mwaka jana, mawaziri wa Kiafrika wa kilimo walikutana nchini Ethiopia kuahidi msaada kwa usalama endelevu wa chakula, kubadili mifumo ya chakula na kujenga mfumo wa uhakika wa biashara na uzalishaji kilimo kutumia mfumo wa Teknolojia katika bara hilo.