Wapiganaji wa upinzani wanasema majeshi ya serikali yamekuwa yakisonga mbele kufikia ngome yao ya mashariki ya Benghazi siku ya Jumamosi, wakati viongozi wa dunia wanakutana mjini Paris kwa mkutano wa dharura juu ya hali ya Libya.
Wajumbe kutoka Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Umoja wa nchi za Kiarabu na Marekani wamemaliza mazungumzo yao mjini Paris juu ya kuzorota kwa hali ya usalama huko Libya.
Akizungumza na waandishi habari, rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy amesema viongozi wa nchi za magharibi wanakubaliana juu ya kutekeleza azimio la Baraza la Usalama la kushambulia ndege yeyote ya kijeshi itakayorushwa juu ya anga ya Libya. Anasema wamekubaliana kuchukua hatua za kijeshi ili kuwalinda raia wa Libya
wajumbe hao walipokuwa wanakutana waasi wa Libya wanasema wameweza kurudisha nyuma kwa kiasi fulani majeshi ya serikali yaliyokua yanasonga mbele upande wa magharibi wa mji wa Benghazi. Wapiganaji wanasema majeshi ya serikali yaliweza pia kutengua ndege yao iliyokuwa inasafiri juu ya mji huo.
Kuna ripoti pia za mapigano kusini mwa Benghazi katika mji wa Adjabiya na Misrata mji wa magharibi unaoshikiliwa na waasi.