Maandamano yaliyoanza Jumanne yameendelea kwa siku ya tatu, licha ya serikali kuondoa sehemu ya mapendekezo ya nyongeza ya ushuru.
Jijini Nairobi, mamia ya waandamanaji walijitokeza wiki hii, wakiwataka wabunge kukataa muswada wa fedha wa 2024, ambao unaongeza ushuru katika sekta mbalimbali za uchumi. Baadhi ya kodi hizo za juu ni matokeo ya deni la miundombinu kutoka China.
Mamia zaidi waliandamana katika mji alikozaliwa Rais William Ruto wa Eldoret, na miji ya Nyeri, Nakuru, Kisii na Kisumu.
Ushuru unaopendekezwa utaongeza bei za taulo za watoto, matairi, betri, simu za kisasa na kamera. Serikali inataka kuongeza ushuru wa mafuta kwa shilingi 9, ambazo wafadhili wa mswada huo wanasema zitatumika kukarabati barabara zilizoharibika.
Serikali pia imeanzisha kile kinachoitwa tozo ya ikolojia, ambayo inasema ni muhimu kupambana na uchafuzi wa plastiki na kulinda mazingira.
Effie Muendo ni mmoja wa maelfu ya waandamanaji ambao wamejitokeza kupinga ushuru uliopendekezwa.
Effie Muendo anaeleza: “Mswada huu ni kinyume na katiba, na adhabu kubwa kwa watu wa Kenya. Asilimia 65 ya wanawake hawawezi kumudu taulo za kujisitiri, na bado wanataka kuzitoza ushuru. Wanatuambia wanataka tununue bidhaa za ndani wakati wanazitoza ushuru mkubwa tutawezaje kuzinunua?”
Maandamano hayo Alhamisi yaliendelea kwa saa nyingi na polisi walitumia maji ya kuwasha na gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wamevamia barabara katikati ya Nairobi. Baadhi ya waandamanaji hawakufurahishwa na uwepo wa polisi, hali iliyowazuia kuingia kwenye majengo ya bunge. Diana anasema haelewi ni kwa nini polisi walikuwa wakiwazuia, lakini wanapigania Kenya bora.
Diana anaeleza: “Wanaturushia gesi ya kutoa machozi, na wanatupiga. Hatuna amani, tunaandamana kwa amani kwa ajili ya nchi yetu kwa sababu tunaipenda Kenya.”
Kimani Mbugua, mwandamanaji mwingine amesema atapambana na muswada huo hadi mwisho.
Mbugua anasema: “Tunatakiwa kuandamana, ni haki yetu kikatiba. Sielewi kwa nini serikali inarusha gesi ya kutoa machozi, na sisi tuko hapa tunatekeleza haki yetu ya kidemokrasia. Tuko hapa kupigania muswada huo kwa sababu ni wa unyonyaji na lazima upigwe vita na lazima ukataliwe.”
Kamati ya bunge inayosimamia masuala ya fedha na mipango imeondoa ushuru uliopendekezwa wa mkate, mafuta ya kupikia, magari kwa kila mwaka ya asilimia 2.5 na miamala ya kifedha. Mabadiliko hayo ya Jumanne hayakuwaridhisha waandamanaji waliotaka mswada huo wote ufutwe. Lakini matarajio hayo hayawafuraishi wanachama wa chama tawala wanaosema kuwa Wakenya wanahitaji kulipa ushuru zaidi ili kufadhili mipango ya maendeleo ya serikali na malipo ya mikopo.
Bunge la taifa linatarajiwa kupigia kura mswada huo wiki ijayo. Wakenya wameapa kuendelea kuandamana huku mjadala ukiendelea.