Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 01:02

Serikali ya Kenya yawasilisha bajeti mpya ikidai itaboresha uchumi


Rais wa Kenya akifanya mahojiano na shirika la habari la AFP mjini Seoul wakati ya mkutano wa Korea Kusini na Afrika Juni 5, 2024. PIcha na Jung Yeon-je / AFP
Rais wa Kenya akifanya mahojiano na shirika la habari la AFP mjini Seoul wakati ya mkutano wa Korea Kusini na Afrika Juni 5, 2024. PIcha na Jung Yeon-je / AFP

Serikali ya Kenya imewasilisha kwenye bunge makadirio ya Bajeti ya mwaka 2024/25 ikitaka takriban shilingi trilioni 3.3 za mapato ya ushuru ili kufadhili bajeti ya pili ya shilingi trilioni 3.91 ya utawala wa Rais William Ruto, ambayo ndiyo kubwa zaidi nchini humo.

Serikali imeweka mgao wa matumizi ya kawaida ya shilingi trilioni 1.5 na matumizi ya maendeleo kuwa shilingi bilioni 727.9 na kuitaja bajeti hiyo kama muhimu kukabiliana na deni la taifa na vile vile kulinda kuimarika kwa uchumi wake.

Bajeti hiyo itakayoambatana na Mswaada wa Fedha wa 2024, utakaoelezea mapendekezo ya serikali ya rais William Ruto ya kuongeza mapato yake ikimulika sekta mbalimbali za uchumi, kwa mujibu wa serikali, inalenga kuendeleza utekelezaji wa haki za kiuchumi na kijamii, kama vile; ufikiaji wa afya kwa wote, kutokomeza njaa, elimu, usafi wa maji na mazingira na kukuza ugatuzi na maendeleo ya usawa, kupunguza gharama ya maisha, kufungua fursa za ajira, kuboresha nafasi ya fedha, kuongeza mapato ya fedha za kigeni, na kukuza ukuaji jumuishi.

Serikali ya Ruto inaitaja bajeti hii kuwa mwelekeo mwema wa uchumi katika nafasi ya ukuaji unaoongozwa na mauzo ya nje huku ikitenga rasilimali za ziada kuwezesha uzalishaji na ukamilishaji wa miradi inayoendelea ya miundombinu.

mafundi wa magari wakifanya matengenezo ya gari katika kiwanda cha magari kilichopo Thika,Nairobi.
mafundi wa magari wakifanya matengenezo ya gari katika kiwanda cha magari kilichopo Thika,Nairobi.

Waziri wa Fedha Njuguna Ndungu akiwasilisha bejeti hiyo ya shilingi trilioni 3.91 Alhamisi katika bunge la Kenya, ameorodhesha mipango mbalimbali ya serikali ya kufikia mapato ya ushuru, kupanua wigo wa kodi na kuzalisha mapato zaidi na vile vile kukopa kiasicha shilingi bilioni 597 kufadhili shughuli za serikali.

Hivyo serikali ya Kenya inatarajia kutekeleza mseto wa hatua za kodi na mageuzi ya sera ya ukusanyaji wa mapato, kuimarisha matumizi ya teknolojia kuongeza wigo wa mapato kupitia ushuru wa kawaida, na pia kutumia teknolojia hiyo kuwakamata wanaokwepa ulipaji ushuru.

Bejeti hiyo inayolenga kufikia mapato ya shilingi trilioni 3.3 ambayo ni asilimia 18.5 ya Pato la Taifa, inatarajiwa kufadhiliwa kwa misaada na mikopo ya masharti nafuu kwa kukopa shilingi bilioni 263.2 sawa na asilimia 1.5 ya Pato la Taifa kutoka vyanzo vya ndani, na shilingi bilioni 333.8 sawa na asilimia 1.8 ya Pato la Taifa kutoka vyanzo vya kigeni, kama njia ya wazi ya kuziba mapungufu kwenye bejeti hiyo yenye kiasi cha shilingi bilioni 597 sawa na asilimia 3.3 ya Pato la Taifa.

Wanunuzi wa bidhaa wakiwa sokoni huko Mombasa
Wanunuzi wa bidhaa wakiwa sokoni huko Mombasa

Makadirio ya ukusanyaji wa mapato ya kodi yanatokana na dhana ya serikali ya Ruto kwamba hatua za mapato zilizomo katika Sheria ya Fedha ya 2023 na Mswaada wa Sheria ya Fedha wa 2024 zitaongeza kasi ya ukuaji wa mapato hadi asilimia 18.8, tofauti na kiwango cha ukuaji wa kihistoria cha asilimia 10, Bw Ndung’u amesema.

Ndung’u anasema kuwa uchumi wa Kenya unakadiriwa kukua kwa asilimia 5.5 mwaka huu 2024, na zaidi ya asilimia 6.0 kwa wastani katika muda wa kati, kutoka 5.3 mwaka wa 2023 na 4.9 mwaka 2022.

Kwa kiasi kikubwa, uchumi wa Kenya unaendeshwa na sekta za kilimo, viwanda, usafiri na uhifadhi, huduma za kifedha pamoja na bima na sekta ya ujenzi.

Serikali inaeleza kuwa ukuaji, uendelevu na maendeleo yaliyopo ya uchumi wake yanathibitishwa na viashiria muhimu vya uchumi kama vile kudhibiti mfumuko wa bei za bidhaa, kuhimili kiwango cha ubadilishaji fedha za kigeni, urari wa malipo, na sera thabiti ya kifedha.

Waziri huyo wa Fedha anaeleza kuwa kwa mwaka wa fedha unaoanza Julai 1, mwaka huu, serikali kuu ina mgao wa shilingi trilioni 2.24, bunge shilingi bilioni 43.6, idara ya mahakama shilingi bilioni 23.69 huku serikali za majimbo zikipata mgao wa shilingi bilioni 400.1.

Aidha, serikali imeweka mgao wa shilingi bilioni 656 kwa sekta ya elimu, shilingi bilioni 126.8 kwa utoaji wa huduma za afya, shilingi bilioni 338.2 kwa sekta ya usalama.

Kuhusu kiwango cha deni la umma, serikali inaeleza kuwa inajaribu kutafuta vyanzo vingi mbadala vya fedha kuondoa mzigo uliopo, ingawa deni hilo linaelekea kima cha shilingi trilioni 11, inataraji kujitolea kulipa deni hilo.

Imetayarishwa na Kennedy Wandera, Sauti ya Amerika, Nairobi

Forum

XS
SM
MD
LG