Katika mkutano wa kwanza kabisa na viongozi wa mataifa 48 ya Afrika, rais Yoon alisema Korea Kusini itaongeza msaada wa maendeleo kwa Afrika hadi kufikia dola bilioni 10 katika miaka sita ijayo huku ikitafuta kunufaika na rasilimali nyingi za madini za bara hilo na uwezekano wake kama soko kubwa la nje.
"Mazungumzo ya Madini Muhimu yaliyozinduliwa na Korea Kusini na Afrika yatakuwa mfano wa mnyororo wa usambazaji thabiti kupitia ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote na kuchangia maendeleo endelevu ya rasilimali za madini kote duniani," Yoon alisema katika hotuba yake ya kufunga mkutano.
Pia aliahidi kutoa dola bilioni 14 katika ufadhili wa mauzo ya nje ili kukuza biashara na uwekezaji kwa kampuni za Korea Kusini barani Afrika.
Korea Kusini ni moja ya wanunuzi wakubwa wa nishati mzalishaji mkubwa duniani wa semikondakta. Pia ni mtengenezaji magari wa tano kwa ukubwa duniani, Hyundai Motor Group, ambayo inafanya jitihada za kuhamia katika magari ya umeme.
Kushirikiana na Afrika, ambayo ina asilimia 30 ya hifadhi za madini muhimu duniani ikiwa ni pamoja na kromi, kobati na manganizi ni muhimu, ofisi ya Yoon ilisema.
Katika tamko la pamoja lililotolewa na Korea Kusini, Umoja wa Afrika (AU) na nchi wanachama wake, viongozi walikubaliana kuharakisha mazungumzo ya makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi na mifumo ya kukuza biashara na uwekezaji.
Pia walitoa wito wa kuendeleza ushirikiano kuhusu usalama wa chakula Afrika kwa msaada wa Korea Kusini kwa kutumia teknolojia ya kilimo cha kisasa.
Viongozi wa Afrika walikaribisha mpango wa Korea Kusini "Tech4Africa" unaolenga kusaidia elimu na mafunzo ya vijana wa Afrika.
Mwenyekiti wa AU na Rais wa Mauritania Mohamed Ould Ghazouani, katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari na Rais Yoon, alisema nchi za Afrika zinatafuta kujifunza kutokana na uzoefu wa Korea katika kuendeleza rasilimali watu, viwanda na mabadiliko ya kidijitali.
SOKO KUBWA NA LINALOKUA KWA HARAKA
Yoon alisema wakuu wa nchi 33 walishiriki katika mkutano huo.
Yoon amependekeza "ukuaji wa pamoja" kama nguzo ya ushirikiano na bara hilo na alisema viongozi walikubaliana kupanua biashara na uwekezaji kwa kuanzisha mifumo ya kitaasisi ili kuwezesha hilo.
Kwa kutoa msaada na miundombinu ya viwanda na mabadiliko ya kidijitali, Korea Kusini inajaribu kunufaika na Afrika ambayo ni soko kubwa na linalokua kwa haraka, bara lenye watu bilioni 1.4, wengi wao wakiwa na umri wa miaka 25 au chini ya hapo.
Tamko la pamoja lilisema viongozi walitambua kutokuwepo kwa utulivu wa njia za usambazaji duniani, na kwamba viwanda vya siku zijazo vinategemea usambazaji thabiti wa rasilimali za madini.
"Katika muktadha huu, tunakubaliana kuzindua Mazungumzo ya Madini Muhimu ya Korea na Afrika wakati wa mkutano huu ambao utakuwa msingi muhimu wa kitaasisi kwa kuimarisha ushirikiano kati ya Korea na Afrika," ilisema.
Park Jong-dae, balozi wa zamani wa Korea Kusini nchini Afrika Kusini na Uganda, alisema mifano ya maendeleo ya nchi za Magharibi na China imeshindwa kukidhi matarajio ya nchi za Afrika, na hivy Korea Kusini inatoa njia mbadala yenye thamani.
"Korea ina uzoefu na maarifa ya maendeleo ... wakati nchi nyingi za Afrika zina uwezekano mkubwa wa maendeleo kulingana na rasilimali ambazo bado hazijachunguzwa, hazijatumiwa, na idadi kubwa ya vijana wenye nguvu," alisema.
Jumatano, viongozi wa biashara wa Korea Kusini wataandaa mkutano wa biashara unaolenga uwekezaji, maendeleo ya viwanda na usalama wa chakula.
Yoon kwa upande mwingine alifanya mazungumzo na viongozi 25 pembeni ya mkutano huo, ofisi yake ilisema.
Yoon alikubaliana na rais wa Tanzania kutoa mikopo ya masharti nafuu ya dola bilioni 2.5 na Ethiopia kwa ufadhili wa dola bilioni 1 kwa ajili ya miundombinu, sayansi na teknolojia na maendeleo ya afya na mijini.
Rais wa Kenya William Ruto alisema Korea Kusini itatoa dola milioni 485 za ufadhili wa maendeleo kwa masharti nafuu.
-Imeandaliwa na Patrick Newman, Sauti ya Amerika, Washington, D.C.
Forum