Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 04:12

Kenya yapokea msaada wa shilingi bilioni 27 kutoka Umoja wa Ulaya


Rais wa Kenya William Ruto alipokuwa Marekani Mei 24, 2024. Picha na ROBERTO SCHMIDT / AFP.
Rais wa Kenya William Ruto alipokuwa Marekani Mei 24, 2024. Picha na ROBERTO SCHMIDT / AFP.

Serikali ya Kenya imetangaza imepokea msaada wenye thamani ya shilingi bilioni 27 kutoka kwa Umoja wa Ulaya, Shirika la Maendeleo la Ufaransa na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya ili kuunganisha nyumba 280,000 kwenye gridi ya umeme chini ya mradi wa usambazaji wa umeme mashinani.

Fedha hizo ambazo serikali ya rais William Ruto inaeleza zinaelekezwa katika jitihada za kufikishia watu wanaoishi mashinani, umeme wa bei nafuu chini ya mradi wa Last Mile unaowezesha kila nyumba ya raia wa Kenya kupata huduma ya umeme,

Msaada huo utasaidia pia mradi wa kuweka nyaya za mtandao wa fiber optic zinazoweza kubeba kiasi kikubwa cha data kupitia huduma za mtandao wa intaneti ili kuwafikia kwa haraka wakazi wa maeneo ya mashambani.

Msaada mwengine wenye thamani ya kiasi ya shilingi bilioni 22 umetolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika, AfDB kwa ubia na Saudi Arabia, vile vile unalenga kuunganisha umeme kwa zaidi ya nyumba 270,000 zilizoko maeneo yasiokuwa na umeme.

Hii ni awamu ya nne ya utekelezaji wa mradi huo na rais Ruto anaeleza ni hatua za wazi za kuziba pengo la maendeleo kati ya jamii zinazoishi mijini na vijijini.

Mpango huo wa Kenya umeelezewa kuwa na lengo la kuwezesha wakazi wote kupata wa umeme ifikapo mwaka 2030.

Ruto ameeleza kuwa mafanikio ya mradi huo yatastawisha biashara katika maeneo ya mashinani na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa na pia kubuni nafasi nyingi za kazi kwa raia wa Kenya.

Rais Ruto akiwa na Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen huko Nairobi Desemba 18, 2023. Picha na LUIS TATO / AFP
Rais Ruto akiwa na Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen huko Nairobi Desemba 18, 2023. Picha na LUIS TATO / AFP

Wakati wa kutia saini mkataba huo, Jumatatu jioni, katika Ikulu ya Nairobi, rais Ruto amesema kuwa serikali ya Kenya, kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita, imeongeza kiwango cha kupatikana umeme kutoka asilimia 27 mwaka wa 2013 hadi zaidi ya asilimia 76 mwaka huu, na nia ya serikali yake ni kuhakikisha nyumba nyingi zinapata umeme wa bei nafuu.

Alex Manyasi, mfuatiliaji wa sera na utendakazi wa serikali, anaeleza kuwa ufanikishaji wa mradi utaleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo, mifumo ya umwagiliaji na makampuni ya usindikaji wa mazao ya kilimo, hivyo kuhakikisha utoshelevu wa chakula.

Mradi huo unaolenga majimbo 32, ukiondoa Nairobi na Mombasa unatarajiwa kukamilika katika muda wa miezi 18.

Walengwa wa mradi huu wanatarajiwa kuchangia kima cha shilingi elfu 15,000 kuunganishwa kwenye gridi ya kitaifa ya umeme, wasioweza kumudi kiasi hicho cha fedha, wanatarajiwa kuchangia kiasi wanachoweza kwa kipindi cha miaka mitatu.

Bw Manyasi, anaeleza kuwa gharama ya kufikisha umeme huo ndio inayokuwa changamoto kubwa kwa familia nyingi, na kwa kiasi kikubwa hulemaza maendeleo.

Uteuzi wa usambazaji wa mitambo ya umeme kwenye mradi huu wa Last Mile unatokana na vigezo vya Hazina ya Kitaifa ya Ustawishaji Maeneo bunge kwa ajili ya ugawaji wa rasilimali.

Serikali kupitia Mamlaka ya Usambazaji Umeme Vijijini, inaunganisha wateja walio karibu na transfoma zilizosakinishwa zinazosambaza huduma za umma kwa gharama sawa ya shilingi elfu 15,000.

Imetayarishwa na Kennedy Wandera, Sauti ya Amerika, Nairobi

Forum

XS
SM
MD
LG