Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres aonya dunia inakabiliwa na hali mbaya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia kikao cha 77 cha Baraza Kuu la UN, makao makuu New York, Sept. 20, 2022.

Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umefunguliwa rasmi Jumanne kwa mkuu wa umoja huo kutoa onyo kali kuhusu "msimu ujao wa baridi wenye malalamiko kote dunaini  kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, kupanda kwa bei za bidhaa pamoja na mizozo inayosababisha mauaji mengi.

Baada ya miaka miwili ya vizuizi kutokana na janga la afya na hotuba kwa njia ya video, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliwataka viongozi kuja kibinafsi kwenye umoja huo ikiwa wanataka kuzungumza, na ni Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky pekee aliyeruhusiwa kutohudhuria binafsi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, wakati akipongeza juhudi za ushirikiano wa kimataifa, ameonya juu ya hali mbaya ya sayari hiyo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutterres akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa likiwa katika kikao chake cha 77.

"Msimu wa baridi duniani uko kwenye upeo wa macho," alisema Guterres wakati akifungua mkutano mkuu wa kila mwaka.

Alitoa wito kwa nchi zote zilizoendelea kiuchumi kutoza kodi kwa faida zinazopatikana kutokana na mafuta ghafi na kutoa fedha hizo kugharimia mambo mawili fidia kutokana na uharibifu unaotokana na mabadiliko ya hali ya hewa na kuwasaidia watu wanaopambana na ongezeko la bei.

"Wachafuzi wa mazingira lazima walipe," alisema Guterres.

Mkutano huo ulibadilika kidogo baada ya kifo cha Malkia Elizabeth II, kwani Rais Joe Biden wa Marekani, kutokana na utamaduni uliopo ni mzungumzaji wa pili katika siku ya ufunguzi wa mkutano, badala yake sasa anatarajiwa kuzungumza Jumatano.

Miongoni mwa viongozi wanaozungumza leo Siku ya kwanza ni pamoja na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, viongozi wa mataifa mawili yenye uchumi mkubwa wa Umoja wa Ulaya, ambayo yamehimiza kuweka vikwazo vikali kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

"Mwaka huu, Ukraine itakuwa juu sana kwenye ajenda. Haitaweza kuepukika," mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell aliwaambia waandishi wa habari mjini New York.

Viongozi wengine watakaozungumza Jumanne ni pamoja na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, ambaye amejitokeza kama dalali kati ya Urusi na Ukraine, ikiwa ni pamoja na kupitia makubaliano ya kusafirisha nafaka inayohitajika sana ulimwenguni.