Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet Alhamisi amemtaka Rais wa Russia Vladimir Putin kusitisha mashambulizi ya silaha dhidi ya Ukraine.”
Akizungumza siku moja baada ya vita hivyo kufikia miezi sita, Bachelet amegusia hali hiyo inayohusisha kinu cha nishati ya nyuklia cha Zaporizhzhia, akisema mapigano katika eneo hilo yanabainisha hatari isiyokadirika kwa raia na mazingira.
Russia na Ukraine zimeshutumiana kutokana na mashambulizi karibu na kinu hicho, na Shirika la Kimtaifa la Nguvu za Atomiki la Kimataifa limesema liko tayari kupeleka timu yake katika eneo hilo kuhakikisha usalama wake.
Bachelet pia alisema Alhamisi kuwa majeshi ya Russia na Ukraine lazima yaheshimu sheria za haki za kibinadamu za kimataifa, wakati jumuiya ya kimataifa lazima ihakikishe inawawajibisha wale wanaozivunja sheria hizo.
Maafisa wa Ukraine walisema Alhamisi idadi ya vifo kutokana na mashambulizi ya makombora ya Russia katika kituo cha treni mashariki ya Ukraine imeongezeka na kufikia watu 25 baada ya miili kadhaa kugunduliwa katika kifusi kwenye mji wa Chaplyne.
“Mashambulizi ya makombora ya Russia yaliyolenga kituo cha treni kilicho kuwa na raia wengi nchini Ukraine inawiana na sura ya mauaji yanayoendelea,” Waziri wa Mambo ya Nje Antony Blinken alituma ujumbe wa Twitter. “Tutaendelea, pamoja na washirika wetu kote duniani, kusimama bega kwa bega na Ukraine na kutaka maafisa wa Russia kuwajibishwa.”
Baadhi ya taarifa katika habari hii inatokana na mashirika ya habari ya AP, AFP, Reuters