Jeshi la Marekani kumshauri Trump juu ya hatua mbalimbali za kukabiliana na Iran

Marekani, Saudi Arabia na Iran

Wizara ya Ulinzi ya Marekani itampa fursa Rais Donald Trump kuchagua hatua mbalimbali za kijeshi ambazo anaweza kutekeleza wakati akifikiria jinsi ya kujibu kile ambacho maafisa wa uongozi wa Marekani wanasema ilikuwa ni shambulizi ambalo halikuwahi kutokea katika vinu vya mafuta vya Saudi Arabia.

Katika mkutano utakaofanyika White House, rais atapewa idadi ya maeneo ambayo yanaweza kushambuliwa nchini Iran, pamoja na njia nyingine za kukabiliana na kitendo hiki cha Iran, na pia atatahadharishwa kuwa hatua ya kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislam ya Iran inaweza kupelekea vita, kulingana na maafisa wa Marekani ambao wanauzoefu na vikao kama hivyo ambao waliweka sharti la kutokutajwa.

Mkutano huo wa usalama wa taifa inawezekana ukawa ni fursa ya kwanza ya kufikiwa maamuzi kuwa Marekani ijibu vipi shambulizi hili lililofanyika dhidi ya mshirika wake mkuu Mashariki ya Kati.

Uamuzi wowote utategemea ushahidi wa aina gani wachunguzi wa Marekani na Saudi Arabia wataweza kukusanya kuthibitisha kuwa makombora na ndege zisizokuwa na rubani zilirushwa na Iran, kama ilivyotangazwa na baadhi ya maafisa akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje Mike Pompeo.

Iran imekanusha kuhusika na shambulizi hilo na kuionya Marekani kuwa shambulizi la aina yoyote litapelekea kutokea vita kamili na hivyo Tehran kulipiza kisasi.

Pompeo na Makamu wa Rais Mike Pence wamelaani shambulio hilo lililofanyika katika vinu vya mafuta vya Saudi Arabia na kusema ni “shambulizi la kivita.” Pence amesema Trump ataangalia ukweli ulivyo, na atafanya uamuzi juu ya hatua zitakazofuatia.

Lakini wananchi wa Marekani waendelee kuwa na uhakika kuwa Marekani itatetea maslahi yetu katika Mashariki ya Kati, na tutasimama bega kwa bega na washirika wetu.”

Marekani katika kukabiliana na shambulizi hilo inaweza kuhusisha hatua za kijeshi, kisiasa na kiuchumi, na hatua mbalimbali za kijeshi zinaweza pia zisihusishe shambulizi la anga kabisa au mashambulizi ya kimitandao ambayo mara nyingi haiwezi kuonekana wazi.

Hatua moja inayoweza kuchukuliwa ni Saudi Arabia kupewa msaada zaidi wa kijeshi katika hatua ya kujihami dhidi ya mashambulizi kutoka kaskazini ya eneo lake, kwani sehemu kubwa ya ulinzi wake umejikita katika eneo ambako kuna uwezekano wa mashambulizi ya wahouthi nchini Yemen kuelekea kusini.