Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 20:46

Marekani, Uswisi zafanya mazungumzo ya faragha


Rais Donald Trump akimkaribisha Rais wa Uswisi Ueli Maurer White House, Washington, Alhamisi, Mei 16, 2019
Rais Donald Trump akimkaribisha Rais wa Uswisi Ueli Maurer White House, Washington, Alhamisi, Mei 16, 2019

Rais wa Marekani Donald Trump amekutana Alhamisi na Rais wa Uswisi Ueli Maurer katika mkutano wa faragha Ikulu ya Marekani, wengi wanaamini mazungumzo hayo yanahusiana na kuongezeka mvutano baina ya Marekani na Iran.

Ikulu ya White House katika tamko lake imesema kuwa Trump alitoa shukurani zake kwa serikali ya Uswisi kwa kusimamia suluhu na mawasiliano ya kidiplomasia kwa niaba ya Marekani,” lakini haikutoa maelezo zaidi.

Iran

Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amefanya ziara, Japan, ambayo ni mshirika wa Marekani na ameituhumu Marekani kwa kuchochea “mvutano.”

VOA imeripoti kuwa wabunge wa Marekani Alhamisi walieleza wasiwasi wao juu ya mvutano huo na Tehran.

Marekani tayari imepeleka manuari katika Ghuba ya Uajemi, na ndege za kivita na vikosi vyake katika nchi zilizoko eneo hilo. Trump ameionya Tehran dhidi ya vitendo vyovyote vya uchokozi.

Ujumbe wa Marekani kwa Iran

Msemaji wa White House Sarah Sanders hakutoa maelezo zaidi juu ya mkutano wa Trump na Rais wa Uswisi lakini alisema rais amekuwa na ujumbe uliokuwa wazi kwa Iran.

“Tutapenda kuona mabadiliko fulani ya tabia yakionekana kutoka kwao. Tutaendelea kuweka shinikizo kubwa kuliko yote na kama alivyosema rais, wakijaribu kufanya uchokozi, hawatapenda kile atachokifanya kujibu hilo,” ameeleza Sanders.

Kevin McCarthy, Mrepublikan wa ngazi ya juu katika Baraza la Wawakilishi la Marekani, amesema uongozi wa Trump unaushahidi wa vitendo vya uchokozi vinavyofanywa na Iran.

Shambulizi la meli, mabomba ya mafuta

“Tunaangalia kile kilichotokea Mashariki ya Kati kwa meli za mafuta za Saudi Arabia. Tunafahamu sasa kwamba kulikuwa na ndege zisizokuwa na rubani zilizoshambulia mabomba ya mafuta. Tunafahamu matamko ya kisiasa yanayotolewa na Iran. Na hivi sasa tunaona uongozi wa Trump inachukua tahadhari kuondosha raia wa Marekani kutoka Iraq, wakiwa hatarini,” amesema kiongozi wa waliowachache (Wareuplikan) katika Baraza la Wawakilishi.

Wamarekani wengi wanakumbuka matamko ya kisiasa kama haya yaliyopelekea kuanza vita nchini Iraq mwaka 2003. Seneta Bob Menendez, Mdemokrat kutoka New Jersey, ameutuhumu uongozi wa Trump kwa kuhodhi taarifa muhimu.

Wahoji kama siyo mtego wa vita

“Hatuhitaji hali mpya ya silaha za maangamivu za Iraq, ambapo tulidanganywa na kuingizwa katika mapigano na Iraq, ikiwa ni moja ya makosa makubwa tuliofanya katika sera yetu ya mambo ya nje. Kwa hiyo hatuwezi kufanya maamuzi ya sera ya usalama ya mambo ya nje na usalama wa taifa bila ya kuwa na taarifa na taarifa za kiintelijensia ambazo zinatufahamisha hatari zilizoko, tathmini ya hatari hizo na tathmini hizo zinanguvu ukweli kwa kiasi gani,” amesema Seneta.

Spika Pelosi amkumbusha Trump

Kiongozi wa waliowengi katika Baraza la Wawakilishi Nancy Pelosi alimkumbusha Trump kuwa huko nyuma alipinga vita vilivyopiganiwa Iraq.

“Moja ya mambo ambayo ninakubaliana na rais ni kuwa sote wawili tunapinga vita iliyopiganiwa Iraq, na ni matumaini yangu kuwa msimamo huohuo utafuatwa na rais wa Marekani, japokuwa baadhi ya wafuasi wake wanamihemuko ya vita,” amesema Spika.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alikuwa Tokyo Alhamisi, ambako ameahidi kuendelea kufanya kazi na Japan katika kuendeleza utulivu katika Ghuba ya Uajemi. Amesema Tehran imetumia “uvumilivu mkubwa” tangu Marekani ilipojiondoa katika mkataba wa nyuklia wa Iran.

XS
SM
MD
LG