Wafanyakazi wa kutoa msaada nchini Indonesia, wameonya kwamba kuna uhaba wa maji safi na madawa kwa maelfu ya wale walioathiriwa na tsunami iliyo sababishwa na mlipuko wa volcano, katika pwani ya nchi hiyo.
Wasiwasi umeongezeka kuhusu uwezekano wa kulipuka magonjwa, waathiriwa wakilazimika kuishi katika kambi za muda.
Kwa mujibu wa ripoti za madaktari, idadi kubwa ya watoto wanaugua homa na kuumwa kichwa, bila ya kunywa maji wala kula chakula cha kutosha.
Tetemeko la ardhi lilofuatiwa na mawimbi makubwa yenye nguvu (Tsunami) iliifunika pwani ya Indonesia na kusababisha uharibifu mkubwa kusini mwa Sumatra na magharibi Java.
Makaazi yaliyo karibu na pwani, pamoja na hoteli za watalii ziliharibiwa vibaya.
Tukio la jumamosi halikuwa limetabiriwa na wataalam sasa wanaonya kwamba matukio Zaidi ya tsunami yanatarajiwa kutokea Indonesia.