EAC inakiri kuchaguliwa Rais Mohamud kunaweza kuishawishi kuipokea Somalia

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud

Kuchaguliwa kwa Rais Hassan Sheikh Mohamud kunaweza kushawishi utawala wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) kuiona nchi hiyo iko tayari kujiunga na jumuiya ya umoja huo, pamoja na kuwa taasisi zake bado zinaendelea kuimarishwa.

Wiki hii, Jumuiya ya Afrika Mashariki iimeanza kutathmini ustahiki wake wa kujiunga na umoja huo. Hatua hii inafuatia historia kukubaliwa kujiunga kwa Sudan kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, zote mbili zikikabiliwa na mzigo mkubwa wa kukabiliana na vita.

Sudan Kusini ilikubaliwa rasmi kujiunga mwaka 2016 lakini imeshindwa kufuata kikamilifu itifaki za jumuiya hiyo.

Kwa mara ya kwanza Somalia iliomba kujiunga na EAC mwaka 2012, lakini ilikataliwa wakati huo, kutokana na misukosuko inayotokana na Al-Shabaab na ukosefu wa sheria thabiti wakati huo.

Wiki iliyopita, katibu mkuu wa EAC, Peter Mathuki alizindua rasmi ujumbe wa kuhakiki hali hiyo na kutathmini kama nchi hiyo iko tayari kujiunga na umoja huo licha ya kuwepo hofu kama vile ilivyokuwa Sudan Kusini na sasa DRC, Somalia inaweza kuwa haipo tayari kujiunga kikamilifu.

Akitetea uamuzi wa ghafla wa kuanzisha mchakato wa kujiunga, Dkt Mathuki alisema Somalia ni muhimu kwa kanda hiyo licha ya kulinganishwa na Sudan Kusini ambayo haijajiunga kikamilifu miaka saba tangu iliporuhusiwa kuingia katika jumuiya hiyo ya kanda.

Kuingia kwa Somalia katika EAC itakuwa muhimu sana kwa sababu masuala yoyote yatakayojitokeza Somalia, labda Al-Shabaab au chochote kile , tunaweza kuvishughulikia katika mfumo wa EAC; linakuwa ni jukumu letu,” alisema Dk Mathuki.

Chanzo cha habari hii ni gazeti la The East African linalochapishwa Kenya.