Utafiti uliofanywa na Umoja wa Mataifa, wizara ya afya pamoja na chuo kikuu cha kitaifa, umefichua kuwa tatizo la afya ya akili limetanda kote nchini. Ripoti hiyo inasema kuwa viwango vya sasa ni asilimia 77 zaidi kulinganishwa na ripoti ya awali kutoka shirika la afya duniani WHO, iliyosema kuwa karibu asilimia 40 ya wakazi wa Somalia walikuwa wanakabiliwa na matatizo ya kiakili.
Ripoti ya sasa pia inaonyesha kuwa tatizo la akili limeongezeka miongoni mwa vijana kulinganishwa na ripoti ya awali. Utafiti wa sasa ambao Umeonyeshwa VOA idhaa ya kisomali, ulifanywa kati ya Oktoba 25 na Novemba 15, 2021. Takwimu hizo zilikusanywa kutoka kwa watu 713 kwenye miji ya Baidoa, Kismayo na Dolow. Kati ya waliofanyiwa utafiti, asilimia 68.1 ni vijana wa chini ya umri wa miaka 35, ambpo asilimia 58.5 walikuwa ni wanaume.