Milipuko na milio ya risasi imesikika katikati ya jiji la Mogadishu siku ya Jumapili.
Walioshuhudia katika mji mkuu wa Somalia walisema walisikia mlipuko mkubwa na kuona wingu la moshi karibu na makao makuu ya manispaa ya Mogadishu majira ya saa sita mchana kwa saa za huko. Jengo hilo ni ofisi ya Meya wa Mogadishu Yusuf Hussein Jimale.
Walioshuhudia katika mji mkuu wamesema walisikia milipuko mingine miwili baada ya ule wa kwanza.
Kundi la wanamgambo wa al-Shabab lilidai kuhusika kupitia ujumbe wa Telegram kwamba wapiganaji wake walifanya shambulio hilo katika makao makuu ya meya. Mashambulizi mabaya ya al-Shabab kwa kawaida yanahusisha kwanza mlipuko yakifuatiwa na waanaojitoa mhanga wenye silaha wanaolenga maeneo.
Serikali ya Somalia bado haijatoa tamko lolote kuhusiana na shambulio hilo. Ofisi ya Meya wa Mogadishu ilishambuliwa na al-Shabab mnamo Julai 24 mwaka 2019 wakati mshambuliaji wa kujitoa mhanga alipomjeruhi vibaya meya wa wakati huo Abdirahman Omar Osman.