Ripoti ya Chuo Kikuu cha East Anglia nchini Uingereza (UEA) amesema majukumu yanayo wakabili wanawake yanaongezeka wakati ambapo wameachwa peke yao kuwatizama watoto na ardhi, wakati wanaume wanaoondoka katika miji yao hawawezi kuwapatia msaada endelevu.
“Kuhama kwa wanaume kunaonekana kama ni mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa – lakini kwa mtizamo wa kijinsia, hausaidii kukidhi mahitaji ya familia na maisha yao,” amesema Profesa Nitya Rao wa UEA, mtafiti aliyeongoza ripoti hiyo.
“Soko la ajira halitoi fursa sawa kwa wanawake. Kwa mfano, huko Afrika Mashariki, wanawake inawalazimu kufanya kazi hatarishi zaidi… Wanajishughulisha na ulanguzi wa dawa za kulevya au biashara ya ngono. Hiyo ndio njia pekee ya kuendesha maisha yao,” mtafiti huyo ameiambia Taasisi ya Thomson Reuters.
Yaliyogunduliwa na tafiti hiyo yanaeleza rai za wataalam wa mashirika mengi ya misaada na hali za dharura, wanaosema wanawake na wasichana wanakabiliwa na madhila yasiyokifani kutokana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
Wakati huohuo, wanaume wanaondoka majumbani aghlabu kutafuta kazi kwa sababu hali ya hewa imekuwa haitabiriki kwa kipindi cha muongo moja uliopita, inakuwa vigumu kupata mavuno kutoka katika kilimo – lakini kuhama huko pia inawezekana kusitatue tatizo hilo, Rao amesema.
“Soko la ajira haliko wazi kwa wafanyakazi hawa maskini na hawapati kazi kwa urahisi,” amesema.
Ukosefu wa mifumo ya misaada inayosimamiwa na serikali na sekta binafsi kwa ajili ya familia zimepelekea wanawake kutojali afya na lishe zao, imesema ripoti hiyo, ambayo imetathmini tafiti 25 kutoka katika maeneo yenye hatari za kuathiriwa na maafa yanayotokana na mabadiliko ya hali ya hewa katika mabara la Afrika na Asia.