Kundi la kimataifa lisilo la kiserikali la Global Witness linaonya kwamba ukataji haramu wa miti unatishia uhai wa moja wapo ya misitu mikubwa duniani huko, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo-DRC. Kundi hilo vile vile linawashutumu wasafirishaji mbao kama vile Ufaransa kwa kutochukua hatua kukabiliana na hali hiyo.
Mtafiti mkuu wa kundi Jules Caron anaandika katika ripoti kwamba si jambo la ajabu kwamba sheria zinadharauliwa huko Congo, lakini kinachoshangaza zaidi ni kwamba Ufaransa haifanyi lolote kusitisha usafirishaji haramu wa mbao.
Akizungumza na shirika la habari la AFP, Caron alisema “tumetumia miaka miwili iliyopita kuchunguza kampuni kubwa ya ukataji miti katika Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo. Inafanya kazi katika eneo lenye ukubwa wa kilomita elfu 40 za mraba . Hiyo ni eneo kubwa kuliko Uswisi na tulichogundua ni kwamba inafanyakazi kinyume cha sheria katika asilimia 90 ya eneo hilo”.
Global Witness inaeleza kwamba imefanya uchunguzi katika harakati za kampuni ya Norsudtimber yenye makazi yake Lictenstien huko DRC kwa miaka miwili.
Inadai kampuni hiyo inafanyakazi zake kinyume cha sheria na ilikiuka vifungu muhimu vya kanuni za msiti nchini kongo na inaeleza kwamba imetumia picha za satelaiti kufuatilia shughuli zake. “Tuligundua pia baadhi ya maeneo yanaonekana kuwepo na uharibifu mkubwa wa mazingira unaosababishwa na kampuni hiyo. Asilimia 60 ya miti inayosafirishwa nje ni ile inayotajwa kuwa katika hatari ya kutoweka na inabidi kulindwa”.
Aidha Global Witness inatoa wito kwa idara ya maendeleo ya Ufaransa kufutilia mbali mradi wa miaka mine wenye thamani ya dola milioni 18 ambayo itakwenda kinyume na malengo ya kuzuia mabadiliko ya hali ya hewa na kulinda msitu na inasaidia makampuni yasiyoheshimu sheria za nchi.
Na ripoti hiyo pia inaonesha kwamba Ufaransa na Norway zinakaribia kuidhinisha pendekezo la kuongezeka mara tatu eneo la kukata miti Congo kufikia kilomita za mraba laki tatu na inasema hilo si wazo zuri kabisa.
Congo ndio mahali inapopatikana asilimia 60 ya msitu mkubwa iliyobanana duniani na ni ya pili kwa ukubwa katika ukanda wa joto baada ya Amazon.