Rais wa sasa wa kikao cha 72 cha baraza kuu la Umoja wa Mataifa Miroslav Lajcak alisema tishio la Marekani kujiondoa kutoka mkataba wa mabadiliko ya hali ya hewa wa Paris limeimarisha dhamira ya nchi wanachama kutekeleza mkataba huo.
Miroslav Lajcak ana ajenda yenye matarajio makubwa kuhusiana na masuala ya kimataifa anayotumai kukamilisha katika mwaka ujao. Kupeleka mbele utekelezaji wa mkataba wa mabadiliko ya hali ya hewa ni moja ya vipaumbele vyake vinne vya juu.
Mwanadiplomasia huyo wa Slovakia aliiambia Sauti ya Amerika-VOA uamuzi wa Marekani kujiondoa kutoka mkataba huo ni jambo la kusikitisha lakini alieleza kwamba azimio hilo limezipa nguvu nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Mataifa kushinikiza utekelezaji wa mkataba huo.
Alisema nchi 40 zitawasilisha mipango yao ya kitaifa ya kupunguza utowaji wa gesi chafu za Greenhouse wakati wa kikao cha 72 cha Umoja wa Mataifa. Kufuatia utawala wa Trump kutangaza nia yake ya kujitoa Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron alitangaza rasmi serikali yake itaendelea kuwa kiongozi wa dunia kwenye suala hili.
“Hivyo basi ninamatumaini sana kwamba tutaweza kufanikisha hili tena kwa kupata uungaji mkono imara kwa mkataba huu. Na ukweli ni kwamba kutokana na majanga ya asili ya karibuni na vimbunga katika kanda ya Caribbean, ninafikiri hilo lipo wazi kwamba mabadiliko ya hali ya hewa ni hatari ya kweli ambayo inaathiri maisha ya watu na tunatakiwa kuchukua hatua zinazostahiki. Na mkataba wa mabadiliko ya hali ya hewa wa Paris ndio jukwaa bora kwa hilo”.
Kipaumbele kingine cha Lajcak ni kuzuia migogoro. Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanajukumu kubwa katika hilo. Kwa mara nyingine Lajcak alisema anasikitishwa na uamuzi wa Marekani kupunguza mchango kwa kazi za kulinda amani za Umoja wa Mataifa lakini aliiambia VOA anaamini hakutakuwa na mwanya katika ufadhili.