Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Januari 24, 2025 Local time: 00:28

Wabunge, Maseneta wavutana juu ya mgao wa fedha Kenya


Mandera County, Kenya
Mandera County, Kenya

Wabunge na Maseneta wiki hii wamejikuta katika mgogoro unaoelezewa na wafuatiliaji wa masuala ya ugatuzi kuwa wenye athari kubwa katika maendeleo ya majimbo.

Lakini wakati pande mbili hizi za utungaji sheria nchini Kenya zikiendelea kuzozana juu ya mgao huo wa fedha kuyawezesha majimbo 47 kuunda bajeti na kutekeleza miradi ya maendeleo na vile vile kuharakisha ulipaji wa mishahara kwa wafanyakazi; wafanyakazi hao wameamua kususia kazi; kiini cha ususiaji kazi ni kucheleweshwa kwa mishahara yao.

Naye Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi wa Majimbo Roba Duba ameeleza hali hii itakuwa na athari kubwa.

Utoaji wa huduma za kimsingi na muhimu katika majimbo zaidi ya ishirini nchini Kenya unatarajiwa kusitishwa Jumanne baada ya wafanyakazi kutangaza amri ya kufanya hivyo.

Wafanyakazi wa majimbo hayo wanalalamikia uchelewashwaji wa mishahara yao huku mgogoro ukiendelea kushuhudiwa kati ya bunge la taifa na la Seneti kuhusu ugavi wa mapato.

Haifahamiki iwapo mahakama ya juu itafikia suluhu juu ya ufafanuzi zaidi wa sheria inayoainisha ugavi wa fedha kutoka serikali kuu katika mzozo huu unaoendelea kati ya mabunge hayo mawili.

Lakini kilicho dhahiri ni kuwa huenda huduma muhimu zikasitishwa na raia wengi wa Kenya katika majimbo haya yasiopungua kumi na tano wakaathirika zaidi.

Magavana nchini Kenya wamekiri kuwa hawana uwezo wa kuwalipa wafanyakazi wanaotoa huduma muhimu kwani bado hawajaanza mchakato wa uundaji bejeti itakayowawezesha kutekeleza miradi inayohitajika.

Baadhi ya majimbo ambayo yanatarajiwa kuathirika na mgomo huu ni jimbo la Kisumu, Murang’a, Isiolo, Marsabit, Kitui, Taita Taveta, Kericho, Nakuru, Elgeyo Marakwet, Embu na mengineyo.

Hata hivyo, mwezi uliyopita, Rais wa Jamhuri ya Kenya Uhuru Kenyatta alikiri kuwa serikali yake haina kiwango cha fedha wanazohitaji magavana na kuwashauri kutumia zile ambazo wamepokea.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Kennedy Wandera, Kenya

XS
SM
MD
LG