Tume ya Taifa ya uchaguzi (CENI) DRC imesema katika tamko lake moto huo uliteketeza mashine za kupigia kura 8,000 kati ya mashine 10,368 zilizokuwa zitumike katika mji mkuu wa Kinshasa, lakini amesema uchaguzi utaendelea kama ilivyopangwa.
CENI haikusema nani inaamini kuwa amehusika na moto huo – ulikuwa umetokea majira ya saa nane usiku katika eneo la Gombe riverside lilioko Kinshasa ambapo ni makazi ya Rais Joseph Kabila – lakini muungano wa vyama tawala na mgombea anaeongoza katika upinzani mara moja walitoa madai ya kulaumiana.
Chama cha Kabila cha Common Front for Congo (FCC) ambacho kinamuunga mkono waziri wa mambo ya ndani wa zamani Emmanuel Ramazani Shadary katika kinyang’anyiro cha urais, kimemtuhumu mgombea wa upinzani Martin Fayulu kwa kuchochea fujo mapema mwezi huu.
“Wakati wa kampeni za uchaguzi zinazoendelea, (Fayulu) amewataka wafuasi wake na wale walio na sikitiko kwake kuangamiza vifaa vya uchaguzi,” FCC ilisema katika tamko lake.
Fayulu ametupilia mbali madai hayo na kusema kuwa vyombo vya usalama inawezekana ndio waliokuwa wamehusika na uchomaji moto huo.
“Moto huo ulizuka katika jengo linalo lindwa na walinzi wa serikali kuu,” Fayulu ameliambia shirika la habari la Reuters.
“Sasa utaelewa kuwa watu wa Kabila hawataki kuandaa uchaguzi.”