Unesco inasisitiza kuwa ulimwenguni bado radio imebakia kuwa ni chombo kinachosikilizwa na watu wengi zaidi.
Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres, katika ujumbe wake mwaka 2020 amesema Siku ya Radio Duniani, sote kwa pamoja tutambue nguvu himilivu ya radio katika kuhamasisha ushiriki wa watu mbalimbali na kujenga dunia yenye amani na yenye kumshirikisha kila binadamu.
Radio inaunganisha jamii
Katika tamko lake Katibu Mkuu anaeleza Radio inawaunganisha watu. Katika zama za mabadiliko ya haraka ya vyombo vya habari, radio bado inaendelea kuwa na nafasi maalum katika kila jamii ikiwa ni chanzo muhimu kinachofikiwa kupasha habari na kutoa taarifa.
Lakini anasema radio pia ni chanzo cha ubunifu ambacho kilipeleka mbele maingiliano na wasikilizaji na kupatikana maudhui inayotokana na watumiaji wa radio miongo kadhaa kabla ya kuwa chombo cha habari cha kawaida.
Radio inatoa sura nzuri ya ushiriki wa watu mbalimbali katika muundo wa matangazo yake, katika lugha zake na kati ya wanataaluma wenyewe. Hii inapeleka ujumbe muhimu kwa dunia, amesema Katibu Mkuu.
"Wakati tukifanya juhudi kufikia malengo endelevu ya maendeleo na kutanzua matatizo ya hali ya hewa, radio inajukumu muhimu la kuwa ni chanzo cha habari na uhamasishaji kwa wakati mmoja," umesema ujumbe wake.
Historia ya Radio
UNESCO ilianzisha Siku ya Radio Duniani mwaka 2011 mara baada ya Baraza Kuu la Unesco kutambua umuhimu wake. Februari 13, 1946, UN ilianzisha Radio ya Umoja huo.
Wachambuzi wa kisiasa wanakubaliana kuwa ni katika kutumia chombo hiki cha mawasiliano na msingi wa kutoa habari radio imekuwa chachu ya kukuza uhuru wa kujieleza na kusukuma mbele haki za binadamu duniani.
Radio ni mawasiliano ya umma ambayo yanawafikia kundi kubwa la wasikilizaji ulimwenguni kote. Bado inatambulika kuwa ni chombo cha mawasiliano chenye nguvu ya ushawishi na kinatumia gharama ndogo zaidi.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa radio iliandaliwa kuzifikia jamii zilizo katika maeneo yaliyoko kando ya miji na vijiji, ambavyo haviwezi kufikiwa kwa urahisi kutokana na matatizo ya barabara na usafiri. Hizi ndizo jamii ambazo zinaathirika zaidi na matatizo mbalimbali. Jamii hizi zinamakundi kama vile, waliokosa fursa za elimu, wenye ulemavu, wanawake, vijana na maskini.
Radio za Kijamii
Radio imeendelea kuwajulisha watendaji mbalimbali matatizo ya jamii kama hizi tulizozitaja kupitia mijadala mbalimbali na kuwapa fursa viongozi kuchukua hatua. Mijadala hii ya umma, inawaunganisha watu bila ya kujali tofauti zao za kielimu. Pia radio husaidia sana kufikisha ujumbe katika hali za dharura na kuwapa taarifa za matumaini kwa waathirika wa majanga mbalimbali, wakati misaada mbalimbali inapokuwa iko njiani kuwafikia.
Lakini kubwa kuliko yote, kuna sura mpya ya radio hivi katika miaka ya hivi karibuni baada ya mawasiliano mbalimbali kuunganishwa. Radio inatumia aina ya teknolojia mpya kama vile simu za mkononi, vifaa ya elektroniki kama vile Tablet, na mitambo yenye nguvu inayosambaza ujumbe mwingi kwa wakati mmoja kupitia mawasiliano ya broadband.