Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 16:11

UN, ILO zaonya wimbi jipya la ajira za watoto kufuatia janga la corona


Mtoto wa miaka 14 analipwa dola 1.24 kwa masaa sita ya kazi ya kuyakarabati matairi ya zamani. PBEAHUMYPAC
Mtoto wa miaka 14 analipwa dola 1.24 kwa masaa sita ya kazi ya kuyakarabati matairi ya zamani. PBEAHUMYPAC

Ripoti ya pamoja ya Shirika la Kimataifa la Kazi, ILO, na Mfuko wa Fedha wa watoto wa Umoja wa Mataifa (UN) imeonya mamilioni ya watoto wanaweza kusukumwa kuingia kwenye ajira za kulazimishwa kwa sababu ya kuzorota kwa uchumi kutokana na janga la COVID-19.

Lisa Schlein anaripoti kutoka Geneva, kwamba mashirika hayo mawili yanazindua ripoti iliyopewa jina, COVID-19 na ajira kwa mtoto wakati wa Mgogoro kuashiria Siku ya Dunia Dhidi ya ajira kwa watoto.

Waandishi wa ripoti hiyo wanaonya janga hili la ulimwengu linaweza kubadili miongo kadhaa ya maendeleo thabiti yaliyofanywa katika kupunguza idadi ya wafanyakazi watoto. Katika miaka 20 iliyopita, ILO inasema ajira kwa watoto imepungua kwa milioni 94.

Takwimu za hivi karibuni zinaweka idadi ya wafanyakazi watoto ulimwenguni kote ni milioni 152, karibu nusu kati ya yao wako kile kinachoitwa ajira ya hatari kwa mtoto. Kazi hizo ni hatari na zinatishia afya ya mwili na akili ya watoto. Ni pamoja na kazi katika sekta za kilimo, madini, ujenzi, viwandani na wafanyakazi wa majumbani.

Ripoti hiyo inaonya kuwa mamilioni ya watoto huenda wakalazimishwa kuingia katika aina mbaya zaidi ya ajira kwani COVID-19 inaharibu uchumi na familia hazina njia ya msaada.

Mtafiti mwandamizi na mwandishi mkuu wa ripoti hiyo ya ILO, Lorenzo Guarcello, ameiambia VOA kwamba ushahidi unazidi kuonyesha kwamba ajira ya watoto inaongezeka kadri shule zinavyofungwa wakati huu wa janga la corona. Anasema watoto wengi ambao hawaendi shuleni wanaweza kulazimishwa kufanya kazi za unyonyaji na za hatari.

Guarcello anasema : "Familia zinatuma watoto kuuza bidhaa barabarani baadhi chakula, maua n.k Kwa hivyo, tayari wanaanza kufanya kazi. Wamewekwa kufanya kazi katika mazingira ya hatari kwa sababu ya kuongezeka, uwezekano wa kuhusika katika sekta isiyo rasmi."

Guarcello ameongeza kusema Afrika ina idadi kubwa zaidi ya wafanyakazi watoto. Kati ya wafanyakazi watoto milioni 72 duniani anasema milioni 31.5 wako kwenye kazi za hatari. Anasema wengi huajiriwa katika sekta ya kilimo.

"Tunajua kuwa kufanya kazi katika kilimo kunaweka watoto katika hali hatari kwa kufanya kazi kwa muda mrefu, kufanya kazi kwenye joto na jua kali kwa siku nzima, kwa kutumia mashine hatari na kadhalika," ameeleza.

Guarcello anasema ILO na UNICEF wanatengeneza mfano wa kuiga ili kuangalia athari za ulimwengu wa COVID-19. Anasema makadirio mapya ya kidunia yatatolewa mwaka ujao.

Miongoni mwa mapendekezo yake, ripoti hiyo ya pamoja inataka usalama kamili wa kijamii na upatikanaji rahisi wa mikopo kwa kaya masikini ili kukabiliana na tishio la ajira kwa watoto.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Sunday Shomari, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG