Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 18:52

UN yatoa dola milioni 40 kupambana na Ebola DRC


Wahudumu wa afya wakiwasili nyumbani kwa mmoja wa wagonjwa wa Ebola nchini DRC.
Wahudumu wa afya wakiwasili nyumbani kwa mmoja wa wagonjwa wa Ebola nchini DRC.

Umoja wa mataifa umetoa dola milioni 40 kusadia Jamhuri ya kidemkrasia ya Congo kukabiliana na maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ebola pamoja na majanga mengine ya kibinadamu kutoka kwenye mfuko wake wa misaada ya dharura.

Kuzuka tena kwa maambukizi ya Ebola kwenye kijiji cha Mbandaka kilichoko kwenye jimbo la Equator wiki moja iliopita kumedumaza matumaini ya kuangamiza janga hilo huko DRC.

Zaidi ya watu 2,200 tayari wamekufa nchini humo tangu kuzuka kwa Ebola kwenye majimbo ya Ituri, Kivu Kusini na Kaskazini mwezi Agosti, 2018.

Wakati hayo yakiarifiwa, misaada ya kimataifa imekuwa ikipungua nchini humo.

Umoja wa Mataifa unaamini kuwa hatua yake ya kutoa dola milioni 40 za dharura itachochea wafadhili wengine wa kimataifa kutoa fedha zaidi kwa DRC.

Kufikia sasa Umoja huo umepokea asilimia 13 pekee za msaada wa dola bilioni mbili zilizohitajika mwaka huu.

Afisi ya Umoja huo unayohusika na maswala ya kibinadamu maarufu, OCHA, imesema kuwa DRC inakabiliana na majanga mengi ya kiafya na kibinadamu kwa wakati mmoja likiwemo la virusi vya Corona.

Msemaji wa afisi hiyo Jens Laerke alisema kuwa janga la covid 19 limeumiza uchumi wa mataifa mengi ulimwenguni huku akiongeza kuwa vita dhidi ya Covid-19 haviwezi kukamilika hadi pale litakapoangamizwa katika kila taifa.

Hata hivyo aliongeza kuwa vita dhidi ya covid 19, haifai kutumiwa kama sababu ya kutoshugulikia majanga mengine ya kibinadamu yanayoendelea kushuhudiwa.

"Lazima tukumbuke kuwa kuna majanga mengine yanayohitaji kushugulikiwa kama vile surua, Ebola, njaa na ukosefu wa lishe bora na ni lazima ufadhili ueendelee kutolewa. Tunaomba wafadhili wa kimataifa kutobagua majanga wanapotoa misaada," alisema.

Kando na Ebola, DRC pia inakabiliana na mlipuko mkubwa zaidi duniani wa surua pamoja na mapigano yaliotorosha maelfu ya watu kutoka makwao hasa mashariki mwa taifa.

Laerke alionya kuwa maswala hayo yasiposhugulikiwa kwa haraka, athari yake huenda ikawa kubwa.

"Watu walioathiriwa watanusurika tu iwapo tutakabiliana na majanga yote kwa wakati mmoja. Itakuwa kazi bure iwapo tutakabiliana na ugonjwa mmoja kwa kuwa mwingine utajitokeza na kuangamiza watu, aliongeza Laerke.

Msaada huo kutoka kwa mfuko wa dharura wa Umoja wa mataifa unatarajiwa kuimarisha mfumo wa afya wa DRC hasa kwa wale waliopona Ebola huku uangalizi ukiongezwa miongoni mwa jamii pamoja na kuwepo kwa mikakati ya kukabiliana na dharura.

Fedha hizo pia zitatumiwa kununua chakula, kujenga makazi, kutoa maji na usafi wa kimazingira pamoja na huduma nyingine muhimu kama kukabiliana na covid 19.

-Imetayayarishwa na Harrison Kamau, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG