Akiwa mjini Ougadougu Jumatano, kiongozi huyo wa Ujerumani alihudhuria mkutano wa viongozi wa mataifa matano ya kanda ya Sahel wa kundi la G5, na kujadili namna ya kuimarisha kikosi maalum cha kupambana na ugaidi katika kanda hiyo ya Afrika magharibi.
Merkel aliahidi msaada mpya wa karibu dola milioni 20 kwa Burkina Faso na nchi yake itatoa msaada wa Euro milioni 60 zaidi kwa kundi la mataifa matano ya Sahel G5 yaliyounda kikosi cha pamoja cha wanajeshi elfu 5 kupambana na ugaidi katika kanda yao.
Amesema Ujerumani itaendelea kuimarisha zaidi msaada huo kwa kutoa vifaa na mchango zaidi wa Euro milioni 10 na vile vile kutakuwa na msaada wa ushauri kupitia jeshi la Ujerumani utaogharimu kati ya Euro milioni 7 hadi 10.
Duru ya kwanza ya mazungumzo yameshafanyika na watu wa kusaidia upande wa jeshi la Ujerumani wamekwisha chaguliwa na ninadhani ushirikiano katika Nyanja hiyo ya jeshi na polisi utaanza haraka na hii ni muhimu kabisa.
Merkel ana mipango pia ya kuipatia Niger Euro milioni 35 kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji binafsi katika kanda hiyo ya Afrika Magharibi kwa msaada wa serikali ya Ujerumani.
Kwa upande wa ushirikiano wa maendeleo tayari tumetoa msaada na ninadhani msaada huo umeanza kufanya kazi vyerma. Mbali na mazungumzo ya Alhamisi katika kiwango cha wakuu wa serikali kutakuwepo pia na mkutano wa kilele kati kati ya mwezi Mei juu ya kazi za wanajeshi ambapo mawaziri wa mambo ya nchi za nje na ulinzi wa Umoja wa Ulaya watakutana na wenzao wa G5. Ujerumani itaisaidia katika mafunzo na uchukuzi.
Lengo la kiongozi wa Ujerumani ni kusaidia kubuni nafasi za ajira bora zaidi kwa ajili ya vijana wa Afrika ili kupunguza hali ya umaskini pamoja na kukabiliana na ukosefu wa utulivu wa kisiasa na ghasia mambo ambayo yanawalazimisha waafrika wengi kukimbilia Ulaya.
Burkina Faso mojawapo ya mataifa maskini kabisa ya Afrika na ni Mwenyekiti wa zamu wa kundi la G5, na hapo Jumatano, Merkel alihudhuria mkutano wa viongozi wa kundi hilo uliohudhuriwa na Marais Ibrahim Boubacar Keita wa Mali, Mohamed Ould Abdel Aziz wa Mauritania, Mahamadou Issoufou wa Niger na Idriss Deby wa Chad. Katika mkutano huo Merkel alitangaza msaada wa Ujerumani wa dola za Marekani milioni 51 kuweza kusaidia kuimarisha usalama katika kanda hiyo.
Angela Merkel amesisitiza : Hivi si vita vya mataifa haya matano pekee yao bali pia ni jukumu na wajibu wa Ulaya, kwani ghasia zitakapotokea, jambo ambalo tunataka kuzuia kwa kila njia, basi athari zake bila shaka zitaenea katika maeneo mengine.
Na ndio manaa anasisitiza kwamba kuna haja ya kutafuta suluhisho la kisiasa kwa Libya kwani hali ya ghasia ikiendelea itakuwa uwanja mzuri mpya wa harakati za kigaidi.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC.