Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 19:15

Mohamed, Nkurunziza kujadili kuondoshwa kwa majeshi ya Burundi


Rais Mohamed Abdullahi Mohamed na Rais Pierre Nkurunziza.
Rais Mohamed Abdullahi Mohamed na Rais Pierre Nkurunziza.

Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Mohamed amewasili nchini Burundi, Jumatatu, katika ziara ya siku mbili.

Rais anatarajiwa kujadiliana na viongozi wa Burundi juu ya suala la kuondolewa wanajeshi wa Burundi waliyoko Somalia kama ilivyopendekezwa na Umoja wa Afrika (AU).

Ratiba ya ziara ya Rais Mohamed Abdullahi Mohamed inaonyesha kwamba atakuwa na kikao na mawaziri wa ulinzi na wakuu wa majeshi ya Burundi na Somalia, na kesho Jumanne Rais Mohamed atakutana ana kwa ana na mwenyeji wake Rais Pierre Nkurunziza.

Taarifa zimeeleza miongoni mwa masuala atakayozungumza na viongozi wa Burundi, kuna lile la kuondolewa kwa wanajeshi wa Burundi elfu moja ambao wanashiriki kwenye kikosi cha umoja wa Afrika cha kulinda amani Somalia, maarufu Amisom.

Kulingana na agizo la Umoja wa Afrika (AU), wanajeshi hao wa Burundi wanatakiwa kuondoka nchini Somalia ifikapo mwishoni mwa mwezi huu wa Februari. Umoja wa Afrika ulieleza awali kwamba hatua hiyo ni katika mchakato wa kuwaondowa wanajeshi wa AU hatua kwa hatua, ili wanajeshi wa Somalia waliopewa mafunzo na kikosi cha AMISOM na wakufunzi wengine kutoka jeshi la Marekani, waanze kusimamia shughuli zote za kulinda usalama wa Somalia.

Pia, AU ilieleza kwamba umelazimika kuitaka Burundi kuanza kuwaondoa wanajeshi wake, sababu kikosi cha Burundi ambacho kinashiriki kwenye jeshi la mseto la AMISOM linaloundwa kwa kiasi kikubwa na wanajeshi kutoka Kenya, Uganda, Ethiopia Burundi, na Djibouti hakina vifaa vya kutosha ili kukabiliana na wapiganaji wa kundi la kigaidi la al-Shabaab.

Lakini Burundi ilipinga agizo hilo la AU, ikisema kwamba makubaliano yaliyoafikiwa na pande zote husika yalieleza kuwa kila nchi itapunguza wanajeshi wake waliyoko kwenye AMISOM kwa kiwango sawa, na kuhisi kwamba imenyongeshwa.

Katika mkutano wa viongozi wa AU uliofanyika Februari 10 -11 mjini Addis Ababa, ujumbe wa Burundi kwenye mkutano huo uliomba bila mafanikio AU kupitia tena uamuzi huo.

Burundi inayo wanajeshi 5,400 kwenye kikosi cha AMISOM chenye walinda amani 20,600. Tangu Umoja wa Ulaya (EU), mfadhili mkuu wa Burundi na mfadhili mkuu wa AMISOM kuiwekea vikwazo serikali ya Burundi, Burundi imekuwa ikitegemea kwa kiwango fulani sarafu za kigeni kupitia shughuli za wanajeshi wake walioko Somalia.

Ripoti zasema, EU kupitia AU umekuwa ukiilipa Burundi kitita cha euro millioni 16 kila baada ya miezi mitatu ambazo ni malipo ya wanajeshi wake wanaoshiriki kwenye kikosi cha AMISOM na kulipia vifaa vya kijeshi vinavyotumiwa na wanajeshi hao.

Wachambuzi wanasema iwapo wanajeshi wa Burundi wataondoshwa nchini Somalia, itakuwa pigo kubwa kwa serikali ya Burundi ambayo tangu mwaka 2015, imekuwa ikikabiliwa na uhaba wa sarafau za kigeni, baada ya EU na wafadhili wake wakuu kama ubelgiji kuiwekea vikwazo vya kiuchumi, kwa kile walichosema kwamba serikali ya Rais Pierre Nkurunziza imeendelea kukiuka haki za msingi za binadamu.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Patrick Nduwimana, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG