Nchi hizo mbili zimejikuta katika mgongano unatokana na mipaka yao ya baharini, ambapo ardhi iliyoko chini ya maji inadaiwa kuwa na kiwango kikubwa cha utajiri wa mafuta na gesi.
Katika tamko lake lililotolewa Jumapili jioni, serikali ya Somalia ilikanusha kwamba ilikuwa imeuza haki ya kuchimba utajiri huo katika mkutano wa mafuta na gesi wa Somalia uliofanyika London Februari 7, na kusema ilikuwa imeonyesha tu ramani ya eneo hilo katika mkutano huo.
Serikali hiyo imesema kuwa haitafanya chochote peke yake katika eneo hilo lenye mgogano mpaka pale kesi itakapoamuliwa na mahakama ya kimataifa ya ICJ huko The Hague. Tarehe ya kusikilizwa kesi hiyo haijapangwa.
Siku ya Jumamosi, Kenya ilimwita Balozi Lucas Tumbo, kutoka Mogadishu kuja Nairobi kufanya mashauriano ya “dharura.”Hatua hiyo imekuja baada ya kile Kenya ilichokiita, katika tamko lake, uamuzi wa kusikitisha na kushtusha… kuvinadi vitale vya mafuta na gesi katika eneo la majini la Kenya ambalo ni mpakani na Somalia.
Kenya pia ilimuamrisha balozi wa Somalia nchini Kenya, Mohamud Ahmed Nur, kuondoka nchini kwenda Somalia kwa “mashauriano” na serikali yake.
Tamko la serikali katika akaunti yake rasmi ya Twitter ililikosea jina la balozi huyo na kumwita Mohammed Muhamud Nur.
Serikali ya Somalia imesema imesikitishwa na uamuzi wa Kenya kumwondoa balozi wake “kabla ya kushauriana na serikali.”
Somalia ilifungua malalamiko katika mahakama ya ICJ Agosti 2014, baada ya serikali ya Mogadishu kusema mazungumzo ya kidiplomasia yalikuwa “hayana tija”. Kenya ilipeleka pingamizi la awali, lakini mahakama ya ICJ iliamuwa Februari 2017 kwamba mahakama hiyo inauwezo wa kusikiliza shauri hilo.
Mahakama hiyo imezitaka nchi hizo zenye mvutano kupeleka hoja ya maandishi ya madai na kupinga shauri hilo mbele yake na itatangaza tarehe ya kusikilizwa kesi hiyo.
Serikali ya Somalia imesema ina nia ya kushirikiana na Kenya kutatua suala hili linaloyakabili mataifa hayo. Kenya imesema mvutano huo unaweza kuhatarisha ushirikiano wao.
Kenya ina maelfu ya wanajeshi wanaolinda amani nchini Somalia ikiwa ni sehemu ya Kikosi cha Umoja wa Afrika kinachopambana na wapiganaji wa al-Shabaab. Tamko la serikali kutoka Nairobi limeeleza pia kuwa Kenya inawapa hifadhi zaidi ya wakimbizi wa Somalia 400,000 na wanaotafuta hifadhi.
Imeonya kuwa ukarimu wa Kenya kwa majirani zake usichukuliwe kama ni jambo lisiyokuwa na uzito wowote.
Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC