Jumla ya watu 1,438 kati ya watu 8,478 waliopimwa waligunduliwa wana virusi hivyo, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na wizara ya afya. Hiyo ni asilimia 17 ya maambukizi, kwa wale waliopimwa.
Tangu nchi hiyo kuingia kwenye wimbi la pili la janga hilo mwishoni mwa mwezi Mei, kiwango kinaonekana kuwa cha wastani wa kati ya asilimia 16 na 19.
Uganda inakabiliana na aina mpya ya virusi ambavyo viligunduliwa kwa mara ya kwanza nchini India, Uingereza, na Afrika Kusini, pamoja na vile vya kwanza, vilivyoripotiwa nchini China.
Kuna wasiwasi kwamba iwapo maambukizi yataendelea kuongezeka kwa kiwango hicho, vituo vya afya vinaweza kukabiliwa na uhaba wa rasilimali muhimu, kama vile oksijen.
Shirika la ndege la Rwanda, jana Alhamisi lilisitisha safari zake kuingia au kutoka Uganda, huku maambukizi yakizidi kuongezeka.
Siku ya Jumatano, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ulisema kwamba wasafiri kutoka Uganda, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hawataruhusiwa kuingia nchini, kuanzia leo Ijumaa.