Mwana wa mfalme Mohammed bin Salman, mtoto wa Mfalme Salman na pia mrithi wa nchi yenye kutoa mafuta zaidi kuliko zote na mshirika mkubwa wa Marekani, amekuwa akijiimarisha kiutawala tangu kumpindua ndugu yake, Mohammed bin Nayef, ambaye alikuwa ndiyo mrithi wa kiti hicho cha ufalme katika mapinduzi yaliyofanyika katika kasri ya mfalme mwaka 2017.
Chanzo cha habari kimesema kuwekwa kizuizini kwa wanafamilia hao kulitokea siku ya Jumamosi. Shirika la habari la Uingereza halikuweza kupata ufafanuzi sababu zilizopelekea kuwekwa kizuizini watu hao.
Gazeti la Wall Street limeripoti kuwekwa kizuizini kwa wana wa mfalme wawili hao mapema Ijumaa, na wameeleza inafungamana na madai ya kuwa wanahusika na jaribio la kufanya mapinduzi.
Maafisa wa Saudi Arabia hawakuweza kupatikana mara moja kutoa maelezo yao mapema Jumamosi. Ofisi ya serikali inayoshughulikia masuala ya habari haikujibu ombi la shirika la habari la Reuters likiwataka watoe maelezo.