Tangazo lao linamaliza mvutano ambao umetishia kuingiza nchi hiyo ya Pembe ya Afrika katika mgogoro mpya.
Viongozi hao wawili walishindwa kukubaliana kuhusu uteuzi wa viongozi wa usalama na kutishia kuvuruga mafanikio ambayo yamepatikana katika kupambana na kundi la wanamgambo.
Katika taarifa ya pamoja, rais Mohamed Abdullahi, na Waziri Mkuu Mohamed Hussein Roble, wamesema kwamba wamekubaliana kuongeza kasi ya maandalizi ya uchaguzi na kutaka serikali za mitaa kuanza maandalizi ya uchaguzi wa mabunge ya chini katika wiki chache zijazo.
Mzozo kati ya viongozi hao wawili ulijitokeza hadharani mwezi Septemba, pale Roble alipomfuta kazi mkuu wa ujasusi wa Somalia, kuhusiana na namna alivyosimamia uchunguzi kuhusu kutoweka kwa afisa mmoja wa ujasusi.
Rais Farmajo, alipuuza hatua ya Waziri mkuu na kumteua afisa wa ujasusi aliyekuwa amefutwa kazi, kama mshauri wake mkuu wa usalama na kutangaza kuondoa mamlaka ya Roble hadi uchaguzi mkuu utakapokamilika.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AFP