Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 22:26

Mahakama ya ICJ yatoa uwamuzi unaopendelea zaidi Somalia kwenye ugomvi wa mpaka na Kenya


Kikao cha Mahakama ya ICJ kikitoa uwamuzi kuhusu ugomvi kati ya Kenya na Somalia
Kikao cha Mahakama ya ICJ kikitoa uwamuzi kuhusu ugomvi kati ya Kenya na Somalia

Mahakama ya Sheria za Kimataifa ya Umoja wa mataifa ICJ, imetoa uamuzi ambao kwa kiwango kikubwa unaunga mkono madai ya Somalia katika kesi yake na Kenya kwenye eneo la Bahari ya Hindi, linalozusha ugomvi kati ya nchi hizo mbili.

Mahakama hiyo imependekeza msitari mpya, ikigawa katikati, sehemu yenye ugomvi licha ya kwamba haina uwezo wa kutekeleza maamuzi yake.

Jopo la majaji 14 wa mahakama ya Umoja wa Mataifa ICJ, katika kikao chake mjini The Hague Uholanzi, siku ya Jumanne limesema kwamba Kenya haijatoa ushahidi wa kutosha kwamba Somalia ilikuwa imefikia makubaliano ya namna mpaka wa sasa ulivyochorwa.

Katika uamuzi wake, mahakama hiyo imegawa katikati sehemu inayogombaniwa na hivyo Kenya kupoteza sehemu ya eneo hilo lenye ukubwa wa kilomita 100,000 mraba.

Uamuzi wa mahakama kwa kiasi kikubwa umeonekana kufurahisha Somali katika kesi ambayo imeonekana kuvuruga uhusiani wa kidiplomasia kati ya majirani hao wawili.

Sehemu yenye mzozo inaaminika kuwa na utajiri mkubwa wa mafuta na gesi.

Kenya inasisitiza kwamba msitari uliochorwa kuelekea mashariki kutoka eneo lililo karibu na Lamu, ambapo kuna mpaka wa Kenya na Somalia, ndio mpaka halisi unaotambuliwa.

Somalia kwa upande wake inasisitiza kwamba mpaka wake unastahili kuwa mstari mstatili jinsi mpaka wake wa ardhi ulivyo

Nchi hizo mbili zilikubaliana mwaka 2009 katika mazungumzo yaliyoungwa mkono na umoja wa mataifa, kusuluhisha mzozo wao wa mpakani kwa njia ya mazungumzo.

Lakini miaka 5 baadaye, Somalia ilielekea katika mahakama ya ICJ baada ya Kenya kuuza leseni za kuchimba mafuta katika sehemu hiyo yenye mzozo kwa kampuni mbili za kimataifa, mwaka 2012.

Kenya imeishutumu mahakama ya ICJ kwa kile imetaja kama mapendeleo na kwamba haitakubali uamuzi wake.

Mahakama ya ICJ haina nguvu za kutekeleza uamuzi wake.

XS
SM
MD
LG