Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 17:40

Raia 40 wa Rwanda wakamatwa kwa tuhuma za ujasusi Uganda


Rais Paul Kagame
Rais Paul Kagame

Rwanda imeeleza malalamiko yake juu ya hatua za maafisa wa usalama wa Uganda kuwakamata raia 40 wa Rwanda jijini Kampala, katika operesheni iliyotekelezwa na maafisa wa ujasusi kutoka jeshini.

Vyombo vya usalama vya Uganda vinasema raia hao wa Rwanda, wanashukiwa kuifanyia ujasusi serikali ya Rwanda.

Wakati huohuo uongozi wa polisi ulikataa kuzungumzia suala hilo, licha ya msemaji wa polisi jijini Kampala kuthibitisha kwa vyombo vya habari Jumatano kwamba ilikuwa inawashikilia raia hao.

Katika mahojiano ya simu na Sauti ya Amerika, msemaji wa polisi maeneo ya Kampala Patrick Onyango, amesema kwa sasa hana uwezo wa kuzungumzia suala hili na kutuelekeza kwa msemaji wa jeshi la Uganda Brigedia Richard Karemera.

Richard Karemeire anasema: “Ndio ni….. hakuna cha kusema kuhusu suala hilo. Kwa wakati huu, sina lolote la kukueleza kuhusu suala hilo.”

Balozi wa Rwanda nchini Uganda Frank Mugambage tayari amewasilisha malalamiko kwa serikali ya Uganda na kusema kuwa ukamataji huo ni dhihaka.

Juhudi za VOA kumfikia Mugambage hazijafaulu, baada ya kutueleza kwamba hawezi kulizungumzia suala hilo.

Naye mchambuzi wa siasa na usalama anayeangazia masuala ya Rwanda na Uganda, Charles Rwomushana, anasema ni vigumu kwa taarifa kutolewa kwa sasa.

Raia hao 40 wa Rwanda, walikamatwa katika Kanisa la Pentecostal Association Churches of Rwanda ADEPR, gorofa ya kwanza, kwenye chumba kilichokuwa sehemu ya burudani.

Haya yanajiri wakati uhusiano kati ya Rwanda na Uganda ni mbaya, kiasi kwamba mpaka kati ya nchi hizo mbili umefungwa.

Kampala inadai kwamba Kigali ina njama za kupindua utawala wa Yoweri Museveni kabla ya uchaguzi mkuu wa 2021.

Rwanda nayo inadai kwamba Uganda imewapa hifadhi watu wanaotaka vile vile kuangusha utawala wa Paul Kagame.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Kennes Bwire, Washington DC.

XS
SM
MD
LG