Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 15:51

Waliokula chakula chenye 'sumu' Uganda waishtaki serikali


Chakula cha msaada
Chakula cha msaada

Familia moja kwa niaba ya familia nyingine kaskazini mashariki mwa Uganda wameishtaki serikali ya Uganda kwa kukosekana chakula na maghala ya kuhifadhia nafaka kitu kilichosababisha nchi kutegemea chakula cha msaada kutoka nje.

Familia ya Isaac Kolimuk na Grace Chepnyorio inayoishi katika wilaya ya Amudat, pamoja na shirika lisilo la kiserikali linalopigania haki ya watu kupata chakula na lile la maisha mema, wanashirikiana katika kesi hii. Kesi hiyo imepangwa kuanza kusikilizwa Julai 29 2019.

Madai ya fidia

Mawakili wao, Daluma na Kwesigabo Walubiri, wamefungua kesi katika Mahakama Kuu mjini Soroti mashariki mwa Uganda wakitaka pamoja na mambo mengine kupewa fidia baada ya chakula cha msaada kusababisha vifo vya watu watatu na wengine zaidi ya 220 kuuguwa na kulazwa hospitali.

Chakula hicho kinadaiwa kuwa kilitolewa na Shirika la Chakula Duniani, WFP, kilichosababisha walaji kuwa na dalili za kuchanganyikiwa, joto jingi mwilini, kuhisi kizunguzungu, kutapika na maumivu ya tumbo.

Athari ya chakula hicho

Familia hiyo kutoka kijiji cha Kadawa, wilayani Amudat, inadai kuwa baada ya kula chakula hicho tarehe Machi 29, 2019, walianza kupiga kelele kwa sauti ya juu huku wakitembea ovyo na kugonga ukuta.

Waathirika hao walipelekwa hospitalini na majirani ambapo uchunguzi wa madaktari ulibaini kwamba chakula walichokula kilikuwa na sumu.

Ripoti za awali katika vyombo vya habari zilieleza madai ya kuwepo sumu katika chakula hicho.

Tamko la Wizara ya Afya

Serikali ya Uganda kupitia Waziri wa Afya Dr. Jane Ruth Aceng, ilieleza kuwa inachunguza kilichosababisha vifo na watu wengine kulazwa hospitalini baada ya kula chakula hicho cha msaada.

Sehemu ya chakula hicho kilipelekwa katika maabara mjini Mombasa Kenya na Johannesburg, Afrika kusini kwa uchunguzi Zaidi na matokeo bado yanasubiriwa.

Shirika la WFP lachukuwa hatua

Japo shirika la chakula duniani WFP lilisitisha utoaji wa msaada wa chakula hicho. Hata hivyo vyanzo vya habari nchini humo vinasema kuna hofu kwamba baadhi ya watu bado wamekificha na kukitumia chakula hicho, kwa sababu ndio chakula pekee walicho nacho.

Familia hizo zinailaumu serikali kwa kuwanyima haki ya kupata chakula cha kutosha kilicho salama na madini muhimu.

Mawakili waibana serikali

Mawakili wanaibana serikali kwa kukosa kulisha watu wake hata baada ya kuahidi kila mara kabla ya kuchaguliwa.

Wanasema, ni jukumu la kila serikali kuhakikisha raia wake wana chakula cha kutosha na kwa bei nafuu na wala sio kutegemea msaada.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG