Papa alikuwa amesimama kwa dakika 10 katika varanda ya hospitali, akitoa shukrani kwa maombi ya kumtakia apate nafuu mapema na akiutakia mema mfumo mzima wa huduma ya afya.
“Nina furaha kuweza kutekeleza miadi yangu ya Jumapili,” lakini mara hii nikiwa hospitali, Papa alisema. “Namshukuru kila mmoja wenu. Nilikuwa nimehisi ukaribu wenu kwangu na msaada wa maombi yenu,” Francis alisema. “Nawashukuru nyote kwa dhati!” alieleza Papa.
Francis, mwenye umri wa miaka 84, amekuwa akipata nafuu vizuri, kwa mujibu wa Vatican, kufuatia upasuaji uliofanywa Julai 4 kuondoa sehemu ya utumbo ambao ulisinyaa kutokana na uvimbe.
Lakini taarifa hiyo haijaeleza lini anaweza kuruhusiwa kuondoka hospitali. Asubuhi baada ya upasuaji huo, msemaji wa ofisi ya Papa alisema kuwa inatarajiwa Papa atakuwa hospitali kwa siku saba, “ili kuendelea na matibabu.”
Hapo awali sauti ya Papa ilisikika kuwa dhaifu wakati alipoanza kuzungumza alipotokea katika varanda nje ya chumba chake maalum katika Hospitali ya Gemelli Polyclinic saa za mchana.
Huo ndio wakati wake wa kawaida anapojitokeza kwenye dirisha lake linalotazamana mukabala na Uwanja wa St. Peters Square. Ikiwa ni wiki moja iliyopita, katika maelezo yake ya mchana ambayo hakutoa fununu yoyote kuwa baada ya masaa machache angelipelekwa kufanyiwa upasuaji usiku ule.
Wakisimama kwenye varanda pamoja naye ni baadhi ya watoto ambao pia wamelazwa katika hospitali hiyo, ambayo ni hospitali kubwa ya Kikatoliki inayotoa mafunzo ya tiba nje ya mji wa Rome. Watu waliokuwa chini walikuwa wakipiga makofi mara kwa mara kumpa moyo.