Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 02:00

Maafisa wa Palestina na Israeli walaani ongezeko la ghasia al-Aqsa


Mwanaume wa Kipalestina akikimbia mabomu ya machozi yaliyofyatuliwa wakati wa ghasia baina ya polisi wa Israeli na Wapalestina, Jerusalem, Jumatatu, Mei 10, 2021. (AP Photo/Mahmoud Illean)
Mwanaume wa Kipalestina akikimbia mabomu ya machozi yaliyofyatuliwa wakati wa ghasia baina ya polisi wa Israeli na Wapalestina, Jerusalem, Jumatatu, Mei 10, 2021. (AP Photo/Mahmoud Illean)

Maafisa wa Palestina na Israeli wamelaani kuongezeka kwa ghasia kwenye uwanja wa msikiti mtakatifu wa al-Aqsa na kwenye mitaa ya Jerusalem Mashariki, huku kila upande ukimlaumu mwengine kwa kusababisha ghasia hizo.

Wakati huohuo Wapalestina na Waisraeli wameandamana Jumatatu kuadhimisha siku ya Jerusalem, au siku ya al-Quds, wakati mji huo ulipotekwa na kukaliwa na Israel wakati wa vita vya siku 6 vya 1967.

Wapalestina wajeruhiwa

Hayo yakiendelea watu 300 wanaripotiwa wamejeruhiwa hii leo pekee yake kutokana na mapambano kati ya polisi na waandamanaji kwenye uwanja wa Mskiti wa al-Aqsa ambao ni eneo la tatu takatifu kwa Waislamu, na la kwanza takatifu kwa wayahudi.

Kwa karibu mwezi mmoja mnamo mwezi huu mtukufu wa Ramadhani Wapalestiina wamekuwa wakipambana wakati wa usiku na polisi wa Israel kwenye uwanja wa al-Aqsa kulalamika dhidi ya hatua kali zilizowekwa na polisi kuingia msikitini humo kutokana na juhudi za kupambana na COVID 19.

ghasia zimezidi mnamo siku za hivi karibuni na maafisa wa afya na chama cha Hilali nyekundu cha palestina wanasema karibu watu 500 wamejeruhiwa mnamo wiki iliyopita wengi wakiwa na majeraha ya risasi za mpira. Mkazi wa Jeruselem aliyejaribu kukaribia msikti huo hii leo anasema walishambuliwa na polisi.

Ghasia za mjini Jerusalem
Ghasia za mjini Jerusalem

Mkazi wa Jerusalem

Mwanzoni waumini walikuwa ndani ya msikiti milango ikiwa wazi halafu mabomu ya kutoa machozi yakafyatuliwa ndani. Watu wakaanza kutaabika. Mimi nilikuwepo kule Bab al Rahma dakika 30 zilizopita na kuanza kutufyatulia gruneti na kututawanya kwa nguvu.

Wapalestina wamekuwa wakiwarushia mawe polisi ambao walikuwa wakijibu kwa kufyatua risasi za mpira na mabomu ya kutoa machozi, ambapo sauti kubwa za mabomu na makelele ya waandamanaji yamekuwa yakisikika hii leo kutokea uwanja mkubwa nje wa mskiti unaochukuliwa na sehemu takatifu na Waislamu na Wayahudi.

Ghasia Mbaya Zaidi

Ghasia hizi zinasemekana ndiyo mbaya zaidi tangu mwaka 2017 huko Jerusalem zilizochochewa na ugomvi wa muda mrefu kutokana na juhudi za walowezi wa Kiyahudi kutaka kuwaondowa Wapalestina waliokuwa wanaishi katika mji wa kale wa Jerusalem tangu mwaka 1956.

Mahakama ya chini ya mji huo ilikubaliana mapema mwaka 2021 na madai ya walowezi kuchukua nyumba za familia 29 katika mtaa wa Sheik Jarr. Lakini Mahakama Kuu iliyokuwa isikilize rufaa dhidi ya kesi hiyo hii leo imeahirisha kikao kufuata ombi la wizara ya sheria kwa hofu ya kuzuka ghasia zaidi.

Mkazi wa mtaa wa Sheikh Jarrah, Nabil Kurd ambako wanaishi familia za Wapalestina wanaotaka kuondolewa anasema Wayahudi hawajabadili mawazo yao.

Kurd anasema : "Wana mkakati uleule wanataka kuwaondoa Wapalestina. Wanatafuta kila njia za kutuondosha sisi Wapalestina. Njia walizokuwa nazo zimefungwa hivi sasa wanatafuta njia tofauti. Lakini sisi tuna ishi hapa katika nchi yetu ardhi yetu. Na hatutakubali kuondoka."

Ghasia hizi zimeenea hivi sasa katika ardhi zote za Wapalestina huko Gaza na Ukanda wa Magharibi pamoja na Jordan. Rais wa Palestina Mahamoud Abass amesema anaunga mkono mashujaa wa al-Aqsa.

Jumuia ya kimataifa imeeleza wasiwasi mkubwa kutokana na ghasia hizo. Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linatarajiwa kukutana hii leo kutokana na ombi la Tunisia kwa kikao cha faragha. Wajumbe wa kamati ya mashirika manne ya Mashariki ya kati yaani Umoja wa Ulaya, Rashia, Marekani na UN pamoja Papa Francis wametoa wito wa utulivu kurudi katika eneo hilo takatifu.

Katibu Mkuu wa UN

Katibu mkuu wa UN Antonio Guterres anasma ni lazima kwa maafisa wa israel kujizuia na kuheshimu haki za watu kukusanyika kwa amani.

Mataifa ya kiarabu pamoja na yale sita yaliyoanzisha uhusiano na Israel, yamelaani utumiaji nguvu unaofanywa na Israel. Marekani pia imeeleza wasi wasi wake kutokana na ghasia hizo.

Waziri Mkuu wa Israeli

Waziri mkuu wa israel Benjamin Neytanyahu alitetea jinsi maafisa wa usalama wanavyokabiliana na ghasia hizo.

Katika juhudi za kuepusha ghasi zaidi Polisi wa jerusalem wamewazuia waisrael kufika kwenye uwanja wa Al Quds hii leo wanapoandamana kuadhimisha siku ya jerusalem .

Msikiti wa al-Aqsa

Uwanja wa msikiti wa al-Aqsa uliyoko katikati ya mji wa kale wa Jerusalem ulitekwa na Israel wakati wa vita vya siku 6 mwaka 1967, pamoja na sehemu yote ya Jerusalem ya Mashariki ambayo ilikuwa chini ya Jordan na baadae kukaliwa na Wayahudi bila ya kutambuliwa na jumuiya ya kimataifa.

Wapalestina wanataka kufanya sehemu hii ya mashariki kuwa mji mkuu wa taifa lao wakati Israeli inadai mji kamili wa Jerusalem ndio mji mkuu wao na huawezi kugawika.

Imetayarishwa na Abdushakur Aboud

XS
SM
MD
LG