Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 01:56

Nchi nyingi duniani zasherehekea sikukuu msimu wa baridi bila masharti ya COVID-19


Sherehe za mwaka mpya katika eneo Times Square, New York, Marekani
Sherehe za mwaka mpya katika eneo Times Square, New York, Marekani

China ilianza kulegeza sera yake ya kutokuwa na kesi hata moja ya covid, maarufu zero-Covid policy mwaka 2022, na inaendelea na sera yake madhubuti ya kutoa chanjo kwa wazee walio katika mazingira hatarishi ambao hawakuchanjwa kwa wingi ikilinganishwa na vijana.

Wiki kadhaa baada ya China kulegeza baadhi ya masharti makali ya kudhibiti Covid 19 duniani, vifo vinavyohusiana na virusi hivyo vimeanza kutokea tena.

Serikali inasema inasitisha kuripoti visa vya wagonjwa wasioonyesha dalili za Covid 19 tangu imekuwa vigumu kuvifuatalia kwa sababu hakuna tena lazima ya kuonyesha uthibitisho wa kupimwa Covid.

Na hiyo haionyeshi wazi namna virusi hivyo vinavyosambaa, au ni vifo vingapi vilivyosababishwa na virusi hivyo.

Wakati China ikikabiliwa na mlipuko wa COVID-19, wananchi walisherehekea Mwaka Mpya mjini Beijing, China Desemba 31, 2022. REUTERS/Florence Lo
Wakati China ikikabiliwa na mlipuko wa COVID-19, wananchi walisherehekea Mwaka Mpya mjini Beijing, China Desemba 31, 2022. REUTERS/Florence Lo

Taarifa kwenye mitandao ya kijamii, kufungwa kwa biashara na ushahidi mwingine unaonyesha idadi kubwa ya watu wameambukizwa.

Wanasayansi kama Profesa Annelies Wilder Smith kutoka London School of Hygiene and Tropical Medicine anaunga mkono hatua mpya za wachina. Anasema sera ya zero-Covid haikuwa endelevu, lakini ni muhimu wazee ambao hawajachanjwa kupata chanjo zao haraka iwezekanavyo.

Profesa Smith anaeleza: “Sasa tunaingia kwenye kile tunachokiita kuondoka kwenye janga. Hii ina maana kwamba tunatoka kwenye janga na kuelekea kwenye hali ambayo siyo janga. Ufafanuzi wa hili ni kwamba kiwango cha maambukizi ambayo tulikuwa tukiyazugumzia maarufu R-nought, kimekifia karibu idadi ya moja au chini ya moja.”

Kuhusu maambukizi, madaktari wanazungumzia Idadi ya R, ambayo ni kipimo cha ukali wa ugonjwa, kwa hiyo idadi ya R ni idadi ya watu ambao wanaweza kuambukizwa na mtu mwenye maambukizi.

Kuingia kwenye hatua ambapo ugonjwa hauitwi tena janga haimaanishi kwamba janga limekwisha, au kwamba kuna nafasi ya kuridhika.

Smith anasema: “Sasa kuna idadi kubwa yaripoti za maandishi na takwimu zinazoonyesha kwamba kwa hakika, ikiwa uliambukizwa Covid, ulikuwa na hatari kubwa ya kupata matatizo mbalimbali. Kwa mfano, hatari ya ugonjwa wa Alzheimer kuongezeka na hatari ya kiharusi, mshutuko wa moyo, lakini hata baadhi ya takwimu zinaonyesha kuna hatari kubwa ya ugonjwa wa kisukari na masuala mengine.”

Sherehe za mwaka mpya mjini, Bangkok, Thailand, Jan. 1, 2023.
Sherehe za mwaka mpya mjini, Bangkok, Thailand, Jan. 1, 2023.

Duniani kote, wanasayansi wana matumaini juu ya kudhibiti virusi vya corona lakini kwa tahadhari, hata katika baadhi ya maeneo ya Ulaya na Amerika yanashuhudia kuongezeka kwa maambukizi ya virusi hivyo na magonjwa mengine ya msimu kama mafua.

Daktari Michael, kiongozi wa Chuo kikuu cha Southampton anasema maeneo mengi ya dunia yanashuhudia viwango vya juu vya wagonjwa wanaolazwa hospitali na msimu wa baridi bado unaendelea kanda ya kaskazini.

Anaonya pia kuwa baadhi ya mabara kama Afrika hayajawa na kiwango cha sawa cha upatikanaji wa chanjo za Covid 19.

Dkt Michael anaongeza kusema: “Kwa mara nyingine, kulazwa hospitali kwa sababu ya Covid 19 nchini Marekani kunaongezeka na itakuwa msimu mgumu wa baridi nchini humo ikijumuishwa na maambukizi ya mafua.

Tunahitaji pia kutafakari, kwa mfano, kusini mwa Jangwa la Sahara, ambako idadi kubwa ya watu hawajapata hata dozi moja ya chanjo ya Covid 19. Hatuna takwimu sahihi ni watu wangapi watakuwa wamepata chanjo katika bara hilo, ikiwa watu wana kinga fulani kutokana na chanjo au maambukizi ya awali. Kwa hiyo, tunahitaji kuboresha ufuatiliaji, kuboresha ukusanyaji wa takwimu barani humo.”

Serikali ya Italia imeamrisha wasafiri wote wanaotokea China kupimwa virusi vya covid-19, Desemba 29, 2022.REUTERS/Jennifer Lorenzini
Serikali ya Italia imeamrisha wasafiri wote wanaotokea China kupimwa virusi vya covid-19, Desemba 29, 2022.REUTERS/Jennifer Lorenzini

Katika miaka ijayo, mwanasayansi huyo anaamini wataalamu wa afya watakabiliwa na janga la kweli la Covid na haitakuwa tu Covid ya muda mrefu.

Linapokuja suala la kufanya utabiri wa mwaka 2023, wanasayansi wanajihadhari, lakini Daktari Michael anaamini kuwa suluhisho linaweza kupatikana baadaye kwa njia ya uboreshwaji mwingine wa chanjo.

Dkt Michael asema: “Tunachohitaji sana ni chanjo ya kizaji kijacho ambayo itapunguza maambukizi ya Covid 19 ili tusiumwe tena. Pengine itapatikana mnamo mwaka mmoja au miwili ijayo. Nadhani tukifikia hatua hiyo pengine tunaweza kusema kuwa tumepunguza kwa kiasi kikubwa Covid 19 kuwa tishio.”

Dkt Michael anasema kuwa makini ni jambo la msingi kwa sababu aina mpya za virusi vya Covid zinajitokeza, mahali ambapo maambukizi hajadhibitiwa.

Anasema virusi hivyo vitakuwa nasi kila mara na tunahitaji kuvifuatalia kwa sababu tunajua kuwa ni virusi hatari. Lakini nadhani tunaelekea mahali pazuri zaidi.

Habari hii inatokana na vyanzo mbalimbali

XS
SM
MD
LG