Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 05:28

Mshukiwa aelekeza gari kizuizi cha ulinzi Bunge la Marekani


Gari lililogonga kizuizi cha moja ya milango ya Bunge la Marekani karibu na jengo la Baraza la Seneti, Washington, Ijumaa, Aprili 2, 2021. (AP Photo/Carolyn Kaster)
Gari lililogonga kizuizi cha moja ya milango ya Bunge la Marekani karibu na jengo la Baraza la Seneti, Washington, Ijumaa, Aprili 2, 2021. (AP Photo/Carolyn Kaster)

Afisa mmoja wa polisi wa Bunge la Marekani ameuawa na mwingine amejeruhiwa Ijumaa wakati dereva mmoja alipovurumisha gari lake na kugonga kizuizi nje ya jengo la Bunge.

Polisi huko Bungeni wamesema mshukiwa huyo alitoka kwenye gari akiwa na kisu mkononi na kuelekea kuwashambulia maafisa wa polisi. Polisi hao walimfyatulia risasi. Mshukiwa huyo ametajwa kuwa ni Noah Green, ana umri wa miaka 25. Polisi wanafanya uchunguzi wa historia yake kupata fununu kilichomsukuma kufanya shambuliz hilo.

Gazeti la Washington Post limeongea na kaka yake Green, Brendan ambaye amesema ndugu yake alikuwa na matatizo ya akili ya afya kwa muda sasa. Ndugu hao wanaishi kwenye nyumba moja huko Virginia. Brendan amesema Noah alimtumia ujumbe wa maandishi Alhamisi baada ya kuondoka nyumbani akisema, “Samahani lakini naondoka na kwenda kuishi ambako sitakuwa na makazi.”

Jarida la Newsweek liliweza kupata baadhi ya ujumbe wa mshukiwa alioweka katika Facebook kabla ya kuondolewa na chombo hicho kikuu cha mawasiliano.

Ujumbe mmoja ulibaini kuwa Green alikuwa mfuasi wa Mhubiri Louis Farrakhan, kiongozi wa kikundi cha Nation of Islam(NOI).

“Mhubiri huyu yuko hapa kuniokoa mimi na binadamu wote, hata kama nitakabiliwa na kifo,” ujumbe huo ulisema.

Kituo cha Kisheria cha Southern Poverty Law, kikundi cha watetezi wa kisheria kinalenga katika maswali ya haki za kiraia na madai ya maslahi ya umma, kilikuwa kimeiorodhesha NOI kama kikundi chenye chuki.

Polisi wamemtaja afisa aliyekufa katika shambulizi hilo kama William “Billy” Evans. Alikuwa ni mmoja wa maafisa katika kitengo cha dharura na mkongwe aliyehudumu katika kikosi cha polisi cha Bunge la Marekani kwa miaka 18.

“Mimi na Jill tulivunjika moyo kusikia shambulizi kwenye kituo cha ukaguzi katika viwanja vya Bunge la Marekani, lililomuuwa afisa William Evans wa Kikosi cha Polisi cha Bunge la Marekani, na pia kumuacha afisa mwenzake akiwa mahtuti,” Rais Joe Biden amesema katika taarifa yake Ijumaa mchana.

Biden, ambaye alipewa maelezo juu ya shambulizi hilo, yuko katika mapumziko ya wikiendi ya Pasaka huko Camp David, sehemu ya mapumziko yar ais iliyoko Maryland. Ameagiza bendera zote White House zipepee nusu mlingoti.

Tukio la Ijumaa lilitokea katika sehemu ya kizuizi cha ukaguzi wa magari Mtaa wa Constitution, upande wa jengo la Seneti la eneo la Bunge la Marekani.

Shambulizi hilo “halielekei kuwa linahusiana na ugaidi, lakini bila shaka tutaendelea kuchunguza,” Robert Contee, kaimu mkuu wa Idara ya Polisi ya Mjini Washington amewaambia waandishi wa habari Ijumaa.

Polisi mjini Washington, kwa kusaidiwa na Idara ya Upelelezi (FBI)

ofisi ya Washington, itaendelea kufanya uchunguzi wa shambulizi hilo la Ijumaa.

“Leo, Marekani imevunjika moyo kwa tukio hili la kusikitisha na kifo cha kishujaa cha mmoja wa maafisa wa polisi wa Bunge la Marekani : Afisa William Evans, “Spika wa Baraza la Wawakilishi Nancy Pelosi amesema katika taarifa yake. “Ni shahidi wa demokrasia yetu.”

Katika ujumbe wa Twitter Ijumaa, kiongozi wa walio wachache katika Baraza la Seneti Mitch McConnell amesema, “Tuwaombee maafisa wa polisi wa Bunge la Marekani ambao wameshambuliwa katika eneo hilo. Bado tunapokea taarifa juu ya kile kilichotokea. Tunawashukuru Polisi wote wa Bunge la Marekani na wale wote wanaoshughulikia hali za dharura ambao wako katika eneo la tukio.”

XS
SM
MD
LG