Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 04:13

Afisa Goodman apewa tuzo kwa kuwanusuru wabunge


Afisa wa polisi Eugene Goodman akiwa katika Bunge la Marekani, Washington, Feb 12, 2021.
Afisa wa polisi Eugene Goodman akiwa katika Bunge la Marekani, Washington, Feb 12, 2021.

Baada ya saa kadhaa za malumbano makali katika kesi ya uchochezi inayomkabili Rais wa zamani Donald Trump, wabunge walipata muda ambao ni nadra kufikia makubaliano.

Fursa hiyo ni ya Baraza la Seneti la Marekani kupiga kura Ijumaa kumtunukia tuzo ya heshima ya juu ya Congress ambayo wanaweza kuitoa kwa afisa wa polisi ambaye alikabiliana na uvamizi wa Bunge la Marekani Januari 6.

Kwa kauli moja waliidhinisha tuzo hiyo, na Baraza la Seneti lilichukua hatua ya kumpa afisa Eugene Goodman wa kikosi cha polisi wa Bunge la Marekani Medali ya Dhahabu ya Congress.

Goodman aliwaongoza waliokuwa wakifanya ghasia katika eneo mbali na kule walikokuwa wabunge wakati genge la wafuasi wa Trump wakifanya uharibifu ndani ya Jengo la Bunge kipindi ambacho bunge lilikuwa linakutana kurasimisha ushindi wa uchaguzi wa Rais Joe Biden.

FILE - Genge la wafuasi wa Rais wa zamani Donald Trump wakivamia Congress.
FILE - Genge la wafuasi wa Rais wa zamani Donald Trump wakivamia Congress.

Katika picha ya video iliyoonyeshwa wakati wa kesi hiyo, Goodman alionekana akimuongoza Seneta Mitt Romney kwenye sehemu yenye usalama.

“Hapa katika kesi hii, tumeona picha mpya za video, video zenye ujumbe mzito, akionyesha utulivu wakati kulikuwa na ghasia, ujasiri wake wakati anatekeleza majukumu yake, uoni wake wa mbali katikati ya ghasia, na utayari wake kukubali kuwa mhanga wa genge lililokuwa na hasira ili tu wengine waweze kuwa salama,” Kiongozi wa walio wengi katika Baraza la Seneti Chuck Schumer, Mdemokrat, alisema mbele ya wajumbe wa Seneti.

Nani walikuwa Wavamizi Ndani ya Bunge la Marekani?

Baada ya wiki tano za uvamizi huo, watafiti wa Chuo Kikuu cha Chicago wamefikia hitimisho kuwa wengi kati ya wavamizi hao katika Congress hawakuwa wanachama wa kikundi cha mrengo wa kulia lakini ni wafuasi wa ‘kawaida’ wa Trump.

Schumer alimtambulisha Goodman, aliyekuwa amesimama nyuma ya ukumbi wa Seneti. Wabunge wote kwa pamoja walisimama kumpa heshima yake Goodman. Goodman aliweka mkono wake sehemu uliopo moyo wake kifuani.

Seneta Chuck Schumer
Seneta Chuck Schumer

Schumer alisema maafisa wote wa usalama waliokabiliana na shambulizi la Congress ni lazima waenziwe na kutambuliwa pia, iliyopelekea wabunge kusimama kuonyesha shukrani zao. Goodman alisimama na wabunge kuwaenzi wenzake.

Kiongozi wa Warepublikan katika Baraza la Seneti Mitch McConnell pia alimpongeza Goodman, akisema : “Kama siyo hasa kwa kufikiri kwa haraka na ushujaa wa Afisa Eugene Goodman, watu katika ukumbi huu wasingeweza kukimbia bila ya kupatwa na madhara siku ile.”

Seneta Mitch McConnell
Seneta Mitch McConnell

Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi aliwasilisha mswaada Alhamisi ambao ungewezesha kutolewa tuzo ya Medali ya Dhahabu ya Congress kwa wafanyakazi wa kikosi cha Polisi cha Congress na Idara ya Polisi eneo la Washington Metropolitan, ambapo maafisa wake waliitwa kwenye tukio kusaidia kuliokoa Jengo la Bunge lililokuwa limevamiwa na wafuasi wa Trump.

Spika Nancy Pelosi
Spika Nancy Pelosi

Trump, rais wa kwanza wa Marekani kukabiliwa na kesi mbili za uchochezi na wa kwanza kukabiliwa na kesi baada ya kuondoka madarakani, amekuwa akituhumiwa kuchochea ghasia kwa hotuba yake ya uchochezi aliyoitoa kwa wafuasi wake muda mfupi kabla ya Bunge la Marekani kuvamiwa na wafuasi wake.

XS
SM
MD
LG