Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 15:21

Kesi inayomkabili Trump yakubalika kikatiba licha ya kwamba ameshaondoka mamlakani - Seneti


Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump
Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump

Kesi inayomkabili Rais Donald Trump kwa shutuma za kuchochea ghasia katika majengo ya bunge mnamo tarehe 6 mwezi Januari mwaka huu, itaendelea kusikilizwa kama ilivyopangwa. Hii ni kufuatia kura iliyopigwa Jumaanne jioni katika ukumbi wa seneti mjini Washington DC, ambapo maseneta waliotaka kesi hiyo iendelee ni 56 huku 44 wakiipinga.

Awali, mawakili wawili wanaomwakilisha Trump walimtetea vikali mteja wao, wakati wa kusikilizwa kwa hoja za mwanzo.

Trump, ambaye baraza la wawakilishi lilimpata na kesi ya kujibu, anashutumiwa kuchochea vurugu na ghasia tarehe 6 mwezi jana.

Kwa masaa mawili, Bruce Castor na David Schoen walitetea hoja yao kwamba kwendelea na kesi hiyo ni kukiuka katiba ya Marekani, na kwamba haifai kwendelea kusikilizwa.

Baraza la Seneti ya Marekani lapiga kura.
Baraza la Seneti ya Marekani lapiga kura.

Hata hivyo, kabla ya muda wao wa kuzunguza kuwadia, viongozi wa mashtaka hayo, ambao ni wajumbe wa baraza la wawakilishi, waliwasilisha hoja mbalimbali kuhusu ni kwa nini ni muhimu kwa kesi hiyo kusikilizwa na kuamriwa haraka iwezekanavyo.

Huku ukumbi ukiwa umetulia, mameneja hao wa kesi walionyesha video za vurugu zilizopigwa siku hiyo ya shambulizi.

Kesi hiyo ya kihistoria ya kumshtaki kwa mara ya pili rais wa zamani wa Marekani Donald Trump, ilianza kusikilizwa Jumanne katika baraza la Seneti.

Trump anashtumiwa kuchochea uasi kwa kuhimiza wafuasi wake kukabiliana na wabunge waliokua katika mchakato wa kurasmisha ushindi wa Joe Biden dhidi ya Trump katika uchaguzi wa Novemba mwaka jana.

"Ingawa tunakubaliana kwamba yaliyotokea tarehe sita ni mambo ya kutia wasiwasi, katiba ya Marekani inaeleza bayana kwamba mashtaka kama haya yanaweza tu kufunguliwa kwa mtu ambaye bado ni rais...na Rais Trump ameshaondolewa mamlakani," alisema Castor.

Karibu wafuasi 800 wa Trump walivamia jengo la bunge na kuvunja milango na madirisha, kupekua ofisi kadhaa za wabunge na kuwashambulia maafisa wa polisi. Watu watano walifariki katika vurugu hizo akiwemo afisa mmoja wa polisi ambaye kifo chake kinaendelea kuchunguzwa kama mauaji yaliyopangwa.

Maseneta 100 wanaosikiliza kesi hiyo dhidi ya Trump wamegawanyika katika makundi ya Wademokrat na Warepublican, na wanasikililiza kesi hiyo wakiwa katika mazingira yasiyokuwa ya kawaida, kwa sababu wengi wao ni mashahidi wa vurugu hizo za tarehe 6.

Ghasia hizo katika jengo la bunge ziliwalazimisha wawakilishi hao kuondoka kikaoni wakihofia usalama wao.

Kura ya theluthi 2 ya maseneta inahitajika ili kumuhukumu Trump, kwa hivyo Warepublikan 17 wanatakiwa kujiunga na Wademokrat 50, jambo ambalo wachunguzi wanasema ni vigumu kuwezekana.

Kesi hiyo itaanza tena Jumatano saa sita za adhuhuri saa za Washington DC.

-Patrick Nduwimana alichangia ripoti hii

XS
SM
MD
LG