Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 03:05

Mfalme wa Saudia ahimiza mataifa makuu duniani kuidhibiti zaidi Iran


Mfalme wa Saudi Arabia Salman
Mfalme wa Saudi Arabia Salman

Mfalme Salman wa Saudi Arabia ameyahimiza mataifa makuu duniani kuchukua msimamo mkali zaidi dhidi hasimu wake Iran wakati inatarajiwa kwamba rais mteule wa Marekani Joe Biden atairudisha tena Marekani kwenye mkataba wa kimataifa wa Nyuklia na Iran uliofikiwa mwaka 2015.

Katika hotuba yake ya kila mwaka mbele ya baraza kuu la kuishauri serikali, Shura, kiongozi huyo wa Saudi Arabia alizungumzia juu ya vita vya Yemen na kutoa wito wa kupatikana suluhisho la mataifa mawili kati ya Israel na Palestina.

Saudi Arabia yenye waumini wengi dhehebu la Suni na Iran ambayo waumini wake ni washia zimekua zikizozana kwa miongo kadhaa, kila mmoja akitaka kuwa na ushawishi mkubwa zaidi katika kanda ya mashariki ya kati. Mataifa yao hasimu yamechukua pia msimamo tofauti katika mgogoro wa Yemen.

Mfalme Salman Bin Abdulaziz alieleza : “Msimamo huu mkali lazima uhakikishe utawala wa Iran umezuiliwa kupata silaha za maangamizi, kuzuiliwa kuendeleza mpango wake wa makombora ya masafa marefu na kutishia amani na usalama.”

Riyadh inaonekana kuwa na wasiwasi kwamba rais mteule wa Marekani Joe Biden anaweza kufufua tena mkataba wa nyuklia wa 2015, uliofikiwa kati ya Iran na mataifa makuu ya dunia, mkataba muhimu uliopatikana wakati Joe Biden alikuwa Makamo Rais chini ya utawala wa Barack Obama.

Rais mstaafu Barack Obama
Rais mstaafu Barack Obama

Lakini Rais Donald Trump ambaye ni mshirika wa karibu wa viongozi wa Saudi Arabia aliindoa Marekani kwenye mkataba huo, na kampeni yake ya kuiwekea shinikizo kubwa Iran, ilipokelewa vyema na Ufalme wa Saudi Arabia.

Rais Donald Trump
Rais Donald Trump

Mfalme Salman vile vile amewashtumu waasi wa Yemen wanaoungwa mkono na Iran kwa kushambulia, mara kwa mara na ndege zisizokuwa na rubani na makombora ya masafa marefu, raia wa Saudi Arabia.

Mfalme wa Saudi Arabia aliongeza kusema :“Tunalani waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran kwa kukiuka sheria za kimataifa na kurusha ndege zisizokuwa na rubani na makombora ya masafa marefu kwenye makazi ya raia wa Saudi Arabia.”

Saudi Arabia inaongoza jeshi la ushirika la nchi za kiarabu dhidi ya waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran katika mgogoro wa miaka mitano nchini Yemen, ambao umeuwa ma elfu ya watu na kulazimisha ma millioni ya wengine kutoroka makazi yao. Umoja wa mataifa umeutaja mgogoro wa Yemen kama janga baya la kibinadamu ulimwenguni.

Mfalme Salman ameelezea kwa mara nyingine uungwaji wake mkono kwa suluhisho la kuwepo mataifa mawili huru, katika mzozo kati ya Palestina na Israel.

Lakini hakuelezea chochote kuhusu mikataba ya hivi karibuni ya kurejesha uhusiano kati ya Israel na washirika wa Saudi Arabia, Bahrain, Umoja wa Falme za Kiarabu na Sudan.

Licha ya uhusiano wa siri na Israel, Saudi Arabia imekataa kutangaza wazi kwamba inalitambua taifa la Israel, bila kupatikana suluhisho la suala la Palestina.

Mfalme Salman ametoa hotuba hiyo siku chache kabla ya kufanyika mkutano wa mataifa yaliondelea kiuchumi duniani (G20), mkutano ambao utaongozwa na Riyadh kwa njia ya mtandao tarehe 21 na tarehe 22 za mwezi huu wa Novemba 2020.

XS
SM
MD
LG