Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 22:09

Masoko ya hisa duniani yatikisika kutokana na uamuzi wa Saudi Arabia


Mwana wa Mfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman.
Mwana wa Mfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman.

Uamuzi wa Saudi Arabia Jumatatu kupunguza bei ya mafuta na kuogeza uzalishaji umezusha wasiwasi mkubwa katika masoko ya hisa kote duniani.

Masoko ya fedha yaliporomoka Jumatatu, yakiburuzwa kutokana na wasiwasi wa bei ya mafuta na athari za uchumi zinazotokana na virusi vya corona vilivyoenea katika nchi zaidi ya 100.

Bei ya mafuta ilishuka kwa asimilia 30 kutokana na kuendelea kutokuwepo makubaliano kati ya wazalishaji wakuu wa mafuta kupunguza usambazaji wa mafuta katika hali ya kupungua kwa mahitaji ya mafuta.

Mkusanyiko wa mashinikizo hayo umepelekea soko la hisa nchini Japan kushuka kwa asilimia 5 Jumatatu, wakati soko la his la Hong Kong Hang Seng lilifunga biashara kwa kushuka kwa asilimia 4 na soko la hisa la Shanghai Composite Index likishuka kwa asilimia 3.

Masoko ya Uingereza, Ufaransa na Ujerumani yote yameshuhudia kushuka kwa kiwango kikubwa kwa hisa siku ya Jumatatu, na hisa za siku za usoni kwa masoko ya Marekani yanaashiria kushuka kwa asilimia 5 yakielekea kufanya biashara Jumatatu.

Wakati dunia ikishuhudia bei za hisa zikishuka wachambuzi wanasema hatua ya Saudi Arabia kupunguza bei hiyo itaathiri zaidi wazalishaji wengine wakuu Duniani ikwemo Marekani na Rashia.

Uamuzi wa Saudi Arabia umechukuliwa baada ya Rashia mzalishaji wa pili mkubwa duniani wa mafuta kukataa pendekezo la umoja wa nchi zinazo safirisha mafuta kwa wingi duniani OPEC kupunguza uzalishaji wa mafuta baada ya bei ya mafuta kushuka.

Kushuka kwa bei kutokana na mlipuko wa ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona.

Nchi za Mashariki ya Kati na Asia zinatazamiwa kufuata hatua ya Saudi Arabia katika juhudi za kuihimiza Rashia kupunguza uzalishaji ili kupandisha bei ya mafuta.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington DC.

XS
SM
MD
LG