Msaada huo wa fedha utakaosaidia chakula kwa wakimbizi waliopo katika kambi za Nduta, Mtendeli na Nyarugusu Kaskazini Magharibi mwa Tanzania, umetolewa na Marekani mjini Dar es Salaam kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa,USAID, kwa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa, WFP, kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania.
Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia utawala wa kambi za wakimbizi na makazi ya wakimbizi, nchini Tanzania Kamishna wa Polisi Nsato Marijan, licha ya kupokea msaada huo amerejea wito wa kuwataka wakimbizi hususan wa kutoka nchini Burundi kurejea makwao kwani kwa sasa nchi hiyo iko shwari kiusalama.
Hata hivyo amesema Serikali ya Tanzania inaendelea kutoa misaada kwenye kambi hizo kwa kushirikiana na Mashirika mbalimbali ya kimataifa kama ilivyoainishwa kwenye mikataba ya kuhudumia wakimbizi.
Balozi wa Marekani Nchini Tanzania Dkt Donald Wright amesema msaada huo kwa wakimbizi umetokana na ukarimu wa watu mbalimbali kwa ajili ya kuokoa maisha ya wananchi ambao wamekuwa waathirika wa mizozo nchini mwao.