Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Novemba 06, 2024 Local time: 03:10

Mapigano yaongezeka kuzunguka kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia


Wakazi wa eneo, wengi wao walikimbia vita, wamekusanyika kukabidhi michango yao ya madawa, nguo, na vitu vyao binafsi kwa ndugu zao katika maeneo yaliyovamiwa na Russia, huko Zaporizhzhia, Ukraine, Aug. 14, 2022.
Wakazi wa eneo, wengi wao walikimbia vita, wamekusanyika kukabidhi michango yao ya madawa, nguo, na vitu vyao binafsi kwa ndugu zao katika maeneo yaliyovamiwa na Russia, huko Zaporizhzhia, Ukraine, Aug. 14, 2022.

Mivutano bado iku juu kuzunguka  kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhia nchini Ukraine, ambapo maafisa wa Ukraine wanayashutumu majeshi ya Russia kwa kuendelea kufyatua roketi kwenye kinu hicho, jambo linalotishia kutokea ajali ya nyuklia.

Majeshi ya Ukraine yatayalenga majeshi ya Russia ambayo yameelekeza mashambulizi katika kinu hicho au kutoka katika kinu hicho, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy alisema katika hotuba yake ya Jumamosi usiku kwa njia ya video.

“Kila mwanajeshi wa Russia ambaye ama anakishambulia kinu hicho, au anafanya mashambulizi na kutumia kinu hicho kama kinga, lazima aelewe kuwa anakuwa ni mlengwa maalum na vyombo vyetu vya kijasusi, kwa ajili ya huduma zetu maalum, kwa jeshi letu,” Zelenskyy alisema.

Pande zote mbili zimeendelea kushutumiana kuhusu mashambulizi ya silaha yanayoendelea karibu na kinu hicho, ambacho kilitekwa na Russia mwezi Machi, muda mfupi baada ya kuivamia Ukraine.

Mwendeshaji kinu hicho ameripoti kuwa mtambo huo uko katika hatari ya kukiuka viwango vya kudhibiti miale na moto baada ya mfululizo wa roketi zinazopigwa ndani na kuzunguka kinu cha nyuklia ambacho ni kikubwa kabisa huko Ulaya tangu wiki iliyopita.

Mwendesha kituo hicho cha nyuklia cha Ukraine Energoatom alisema kituo cha hewa ya nitrogen-oxygen, stesheni ya kusukuma maji machafu katika eneo, pamoja na jengo jirani limeharibiwa vibaya sana katika mashambulizi hayo, na pia “sensa tatu za kupima kiwango cha miale” kuzunguka eneo kavu la kuhifadhi nishati ya nyuklia iliyotumika.

Mwendesha mtambo huo alisema kituo cha idara ya zima moto ambayo iko nje ya kinu hicho pia kilishambuliwa. Maafisa pia walisema bomu lilipiga katika transfoma ya umeme, ikitishia gridi ya usambazaji umeme nchini.

Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki alisema kuna “hatari ya kweli ya janga la nyuklia kutokea” iwapo vita havitasitishwa, na wakaguzi kuruhusiwa kuingia katika mitambo hiyo.

Umoja wa Mataifa unataka haraka upewe ruhusa ya kuingia katika kinu hicho cha nyuklia, wakati maafisa wa Ukraine wakisema majeshi ya Russia yamerusha roketi zaidi ya 40 katika mji wa Marhanets, ambao uko upande wa pili wa Mto Dnieper kutoka kwenye kinu cha nishati.

XS
SM
MD
LG