Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Desemba 27, 2024 Local time: 17:01

Russia na Ukraine zatuhumiana kuhusika na kushambulia kinu cha nyuklia


FILE - Mwanajeshi akiwa na bendera ya Russia katika unifomu yake akilinda karibu na Kinu cha Nyuklia cha Zaporizhzhia katika mkoa wa Zaporizhzhia region, Ukraine, Aug. 4, 2022.
FILE - Mwanajeshi akiwa na bendera ya Russia katika unifomu yake akilinda karibu na Kinu cha Nyuklia cha Zaporizhzhia katika mkoa wa Zaporizhzhia region, Ukraine, Aug. 4, 2022.

Umoja wa Mataifa, unataka ruhusa ya haraka  kuingia katika kinu cha  nyuklia wakati Russia na Ukraine  kwa mara nyingine Ijumaa zimeshutumiana kwa kupiga mabomu karibu na kinu hicho.

Maafisa wa Ukraine walisema majeshi ya Russia yalifyatua zaidi ya roketi 40 katika mji wa Marhanets, ambao uko upande wa pili wa Mto Dnieper kutoka katika kituo hicho cha umeme.

Gavana wa mkoa huo, Valentyn Reznichenko, alisema raia watatu, akiwemo mtoto wa miaka 12, walijeruhiwa katika shambulizi.

Russia inaishutumu Ukraine kwa kufanya shambulizi katika kitu hicho.

Mapigano makali na urushaji mizinga katika eneo la kituo hicho yameripotiwa Ijumaa.

Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki alisema kuna “hatari ya kweli ya janga la nyuklia” hadi pale vita vitakaposimama na wakaguzi wakaruhusiwa kuingia katika eneo hilo.

“Huu ni wakati wa kuwa makini, wakati muhimu, “Mkuu wa IAEA Rafael Grossi alisema Alhamisi jioni wakati wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. “IAEA lazima haraka iruhusiwe kupeleka timu huko Zaporizhzhia.”

Majeshi ya Russia ambayo yanakalia kwa mabavu kinu hicho yameshutumiwa kulitumia eneo kama kinga wakati wakishambulia maeneo ya kijeshi ya Ukraine. Mashambulizi makali katika eneo karibu na kinu hicho yameripotiwa katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Wanajeshi wa Russia wanadhibiti kinu hicho, lakini wafanyakazi wa Ukraine wanaendelea kuendesha kinu hicho.

“Tunajua kuwa majeshi ya Russia yamekuwepo huko kwa muda sasa. Pia tunafahamu kuwa wanajeshi wa Russia wamefyatua mizinga, nafikiri hasa roketi, kutoka eneo linalozunguka kinu cha nishati,” afisa wa ngazi ya juu wa jeshi la Marekani amewaambia waandishi wa habari Ijumaa, akikanusha madai ya Russia kuwa kinu hicho kimekuwa kikilengwa kwa mashambulizi na majeshi ya Ukraine.

“Siamini kabisa kuwa Waukraine, ambao wanajua vyema athari zipi zitapatikana kwa kukipiga kinu cha nishati, wana maslahi yoyote ya kukipiga kinu hicho cha umeme,” afisa huyo ameongeza.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres ameonya katika taarifa yake kuwa kinu cha nishati ya nyuklia cha Zaporizhzhia “ni lazima kisitumike kama sehemu ya operesheni zozote za kijeshi.”

“Makubaliano ya haraka yanahitajika katika kiwango cha kiufundi kwa kuweka eneo salama lisilotumika kijeshi kuhakikisha usalama wa eneo lote,” ameeleza zaidi.

Katika maendeleo mengine, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy Ijumaa aliisihi Marekani na nchi nyingine kuitambua Russia kama taifa linalodhamini ugaidi, akisema katika hotuba yake kwa njia ya video usiku, “baada kila walichofanya wavamizi nchini Ukraine, kuna njia moja tu ya kukabiliana na Russia – kama taifa la kigaidi.”

Afisa wa ngazi ya juu wa Russia alisema Ijumaa kuwa mahusiano kati ya Moscow na Washington yataharibika vibaya sana endapo Baraza la Seneti la Marekani litapitisha sheria ya kuitambua Russia kama ni taifa linalodhamini ugaidi.

Sehemu ya ripoti hii inatoka mashirika ya habari ya Reuters, AP, AFP

XS
SM
MD
LG