Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 29, 2024 Local time: 11:33

Kwa nini Marekani Siku ya Wafanyakazi inasheherekewa Septemba?


FILE - Watoto wakifanya kazi katika kiwanda cha kutengeneza matofali nje ya mji wa Jamuu, India Mei 1, 2018.
FILE - Watoto wakifanya kazi katika kiwanda cha kutengeneza matofali nje ya mji wa Jamuu, India Mei 1, 2018.

Siku ya Wafanyakazi ni sikukuu ya kitaifa, iliyoanzishwa kuwaenzi wafanyakazi wa Marekani na michango yao katika uchumi.

Wamarekani wengi wanaitumia siku hii kuadhimisha kumalizika kwa kipindi cha joto na unaweza kustaajabu kujua kuwa siku hii chimbuko lake linatokana na harakati za wafanyakazi mwishoni mwa mwaka 1800.

Vipi sikukuu hii ilianza?

Mnamo miaka ya 1800, mapinduzi ya viwandani ndiyo yalikuwa yamefikia kileleni, na Wamarekani walikuwa wanafanya kazi masaa 12 kwa siku, siku saba kwa wiki katika mazingira magumu na malipo duni. Hata watoto wadogo walikuwa wanafanya kazi viwandani. Takriban hakuna mwajiri aliyetoa likizo ya ugonjwa kwa wafanyakazi, kulipa likizo ya kawaida au maslahi ya afya.

Kadiri wafanyakazi walivyokuwa wanaendelea kujipanga zaidi katika vyama vya wafanyakazi walianza kuandamana kupinga hali mbaya na hatarishi za maeneo ya kazi na kushawishi maslahi zaidi kutoka kwa waajiri wao.

Hatua hiyo ya kuwatambua wafanyakazi kwa kuwapa likizo ilianza na serikali za majimbo, na moja baada ya mwengine, akapitisha sheria kumuenzi mfanyakazi wa kawaida.

Bunge la Marekani lilianzisha sikukuu ya wafanyakazi kitaifa Juni 28, 1894, na kuweka Jumatatu ya kwanza ya mwezi Septemba kuwa Siku ya Wafanyakazi.

Tofauti ya Siku ya Wafanyakazi na siku ya Mei Mosi

Vyote viwili Siku ya Wafanyakazi na Siku ya Kimataifa ya Wafanyakazi, au siku ya Mei Mosi, vinamuenzi mfanyakazi wa kawaida. Mei Mosi, ambayo huwa inaadhimishwa zaidi katika nchi zenye viwanda ulimwenguni, ilianza kwa sababu ya matukio yaliyojiri Marekani.

Mwezi Mei 1886, maandamano ya wafanyakazi yalifanyika katika Bustani ya Haymarket iliyoko Chicago kushinikiza kazi zifanywe kwa masaa nane. Bomu liliripuka katika maandamano hayo na kumuua afisa wa polisi na raia wanne. Tukio hilo lilifanya habari hiyo kuvuma ulimwenguni na siku hiyo ikawa ni maadhimisho ya kila mwaka ya maandamano ya wafanyakazi ulimwenguni kote.

Kwa nini Wamarekani hawaadhimishi Mei Mosi?

Kufuatia tukio hilo la Haymarket, upinzani mkubwa dhidi ya harakati za umoja wa wafanyakazi uliiibuka nchini Marekani. Baada ya miaka kadhaa, Mei Mosi ikawa inanasibishwa na siasa za mrengo wa kushoto, wakati Siku ya Wafanyakazi, ilikuja kuongezeka kutambuliwa na manispaa na majimbo.

Wakati Marekani ilipokuwa inadhamiria kuanzisha sikukuu ya kitaifa ya wafanyakazi, Rais wa Marekani Grover Cleveland hakutaka kuchagua siku ya tarehe halisi ya Mei Mosi kwa sababu ya kuhusishwa siku hiyo na mlipuko wa bomu huko Haymaker, na badala yake akachagua siku mbadala ya maadhimisho hayo mwezi Septemba.

XS
SM
MD
LG