Kwa mujibu wa gazeti la The East African nchini Kenya hivi sasa meli chache zaidi zinawasili na safari nyingi kusitishwa wakati nchi mbalimbali duniani zinaweka vizuizi vya kusafiri ili kudhibiti marahdi ambayo yametangazwa kuwa janga la kimataifa.
Hadi sasa, bandari hiyo imepokea taarifa za kusitishwa safari za meli 37 ambazo zilikuwa zimepangwa kuingia katika bandari ya Kenya mwezi wa Machi, wakati hatma ya meli 104 haijaweza kujulikana.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari ya Kenya Daniel Manduku amesema hata meli hizo chache ambazo zimewasili bandarini hapo mapema mwezi Februari, zimefikisha kiwango kidogo sana ikiathiri kiasi cha mzigo uliokuwa unatarajiwa.
Mkuu wa KPA amesema japokuwa bado hawajafanya tathmini kujua kiwango cha hasara ya kibiashara, iwapo janga hili la corona halitadhibitiwa mapema, wanatarajia kupungua zaidi kwa idadi ya meli, hususan kutoka China.
Lakini, kuanzia wiki hii, China imerikodi idadi ya chini ya maambukizo mapya na viwanda vinafunguliwa kote nchini humo. Bahati mbaya hili linatokea wakati mgonjwa wa kwanza anaripotiwa nchini Kenya na wengi wengine ulimwenguni.
China ni chanzo pekee kikuu cha soko la Kenya, ikichangia moja ya tano ya bidhaa zinazoingia nchini kila mwaka.
Bidhaa zilizoingia Kenya kutoka China mwezi Januari hadi Novemba 2019 zilifikia thamani ya dola za Marekani milioni 32.5, au asilimia 20.3 ya malipo ya bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 16 zilizoingizwa nchini, ikiwa ni chini kidogo ya dola milioni 34.6 mwaka 2018 kutokana na kupungua kwa bidhaa zinazoagizwa nchini za mashine zinazotumika kwa ajili ya Reli ya SGR.
“Kenya hupokea zaidi ya asilimia 40 ya bidhaa zake zinazoagizwa kutoka China na kwa vile usafirishaji wa meli ni biashara ya kimataifa, imeathiri idadi ya meli zinazosafirisha mizigo na matukio yake biashara kuwa katika hali mbaya.”
Afisa mtendaji mkuu wa Chama cha Waagizaji Biashra na Wafanyabiashara wadogo Samuel Karanja amesema kuwa wamepoteza karibuni dola milioni 300 tangu kuanza kwa maambukizi ya kirusi cha corona kwani bidhaa zimekwama nchini China.
Kenya ni kituo cha usafirishaji Afrika Mashariki, inayohudumia bidhaa zinazotoka nje ya nchi ambazo hazina bandari kama vile Uganda, Rwanda, Sudan Kusini, Burundi na DRC, kuzorota kwa shughuli za bandari bila shaka kutaathiri nchi za jirani yake.