Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 16:29

Kenya kuzindua safari zaidi za ndege kutoka Ulaya, Mashariki ya Kati


Waziri wa Utalii Najib Balala
Waziri wa Utalii Najib Balala

Serikali ya Kenya imetangaza kuingia mikataba na mashirika ya ndege za kimataifa, ili kuzindua safari zaidi za moja kwa moja kutoka mataifa ya Ulaya na nchi za Kiarabu.

Mipango hiyo imetangazwa na Waziri wa Utalii Kenya, Najib Balala, alipofungua rasmi Kongamano la Utalii la Kimataifa – SKALl CONGRESS, ambalo limeanza Alhamisi katika mji wa Mombasa.

Waziri wa Utalii nchini Kenya Najib Balala alifungua rasmi kongamano hilo, akitangaza kuwa Kenya imefungua milango yake kukaribisha mashirika zaidi yanayo miliki ndege za kimataifa, kufanya safari za moja kwa moja hadi Mombasa.

Alisema, kwa mfano ndege hizo zikitokea miji ya Doha-Qatar, Brusssels-Ubelgiji, Amsterdam – Uholanzi, na hapo mwaka 2019 kutakuwa na ndege ya moja kwa moja kutoka London hadi Mombasa.

Waziri Balala amesema vikwazo vya usafiri vilivyowekwa awali na mataifa makubwa ulimwenguni kwa sababu ya vitisho vya magaidi, vilikwamisha mambo mengi kufanyika Kenya….

Kongamano la Utalii wa Kimataifa

Rais wa Kongamano la kila mwaka la Utalii wa Kimataifa – Skal Congress, Susanna Saari, ambaye ni raia wa Finland, amehutubia watalii zaidi ya 400 kutoka nchi 40 waliofika Mombasa kuhudhuria kongamano hilo.

Baadhi ya watalii waliohojiwa na Sauti ya Amerika wamesema lengo kuu ni kujenga utamaduni baina ya mataifa ya ulimwengu kupitia utalii na safari kama hizi, wakiamini kuwa hii pia ni njia ya kudumisha amani na usalama duniani.

Hafla hii iliyo wavutia watalii wa ndani na wale wa nje imeshuhudia waandaaji wa Skal Congress wakitoa tuzo kwa Klabu za Watalii na wadau wengine waliotoa mchango-mkubwa sehemu tofauti duniani.

Miongoni mwa washindi wa mwaka huu ni pamoja na Klabu bora iitwayo Bahius kutoka Mexico, Boston Club kutoka Marekani, na Hifadhi wa wanyama ya Zululand kutoka Afrika Kusini.

Kati ya mataifa 40 yanayo wakilishwa hapa Mombasa, watalii wanatoka nchi 8 za Afrika – Zimbabwe, Ethiopia, Nigeria, Ghana, Afrika Kusini, Uganda, Tanzania, na wenyeji wa Kenya.

Kongamano hili litaendelea kwa siku 4,ambapo watalii watapata fursa ya kutembelea mbuga za wanyama, maneo ya kihistoria, hoteli za kifahari, na mwisho kuwachagua viongozi wapya.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Josephat Kioko, Kenya

XS
SM
MD
LG