Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 21, 2024 Local time: 17:18

Uingereza yataka Kenya iongeze ulinzi Laikipia


Balozi wa Uingereza nchini Kenya Nic Hailey
Balozi wa Uingereza nchini Kenya Nic Hailey

Serikali ya Uingereza Jumatatu imeitaka serikali ya Kenya kuongeza ulinzi katika kaunti ya Laikipia ambako raia wake aliuawa na wafugaji Jumamosi usiku.

Mwili wa Tristan Voorspuy, mwenye uraia pacha wa Kenya/Uingereza, ambaye ni moja wa wamiliki wawili wa eneo hilo, umepatikana katika ranchi ya Sosian.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Kenya, kabla ya kuuwawa Voorspuy alipanda farasi katika ziara yake kuelekea kwenye ranchi ambako nyumba mbili zilikuwa zimechomwa moto.

Kurejesha Utulivu

Katika tamko kwa vyombo vya habari Jumatatu, balozi wa Uingereza nchini Kenya Nic Hailey,amesema “amesikitishwa sana kwa mauaji hayo.”

“Naendelea kuhimiza vyombo vya dola vya Kenya kuchukua hatua muhimu kwa haraka kurejesha utawala wa kisheria na utulivu, na kulinda usalama wa wananchi na mali zao katika eneo hilo.”

“Nilikuwa nimesikitishwa na mauaji ya Tristan Voorspuy. Ubalozi wa Uingereza unaendelea kufanya mawasiliano na familia ya marehemu kuwapa msaada katika wakati huu mgumu,” amesema Hailey.

Amesema katika miezi kadhaa iliyopita “nimerejea kutuma ujumbe kwa vyombo vya dola vya Kenya kwamba Uingereza ilikuwa ina wasiwasi mkubwa juu ya usalama katika baadhi ya maeneo huko Laikipia.

“Nimefanya hivyo mara nyingine tena kufuatia mauaji ya Voorspuy,” balozi wa Uingereza amesema.

Ameridhika na nia ya dhati ya viongozi wa juu katika juhudi ya kutatua tatizo hilo.

Serikali ya Kenya Jumatatu imewahakikishia watalii wa kimataifa wanaotembelea Laikipia kwamba maeneo ya hifadhi na ranchi nchini ni salama kwa safari zozote.

Polisi Kusindikiza Misafara

Msemaji wa polisi Charles Owino amesema kuwa ulinzi umeimarishwa nchini kwa ajili ya kuwalinda wageni, wawekezaji na maeneo ya utalii, zikiwemo kambi na sehemu za malazi.

Ameongeza kuwa polisi wamekuwa wakitoa ulinzi kwa magari yanayowachukua watalii wanaotembelea ranchi na hifadhi ili waweze kufurahia safari zao za kwenye mbuga bila ya kuwa na wasiwasi juu ya usalama wao.

Owino amesema mpaka sasa hakuna mtalii yoyote aliathirika na uvamizi wa wafugaji katika ranchi hizo.

Amesema maafisa kutoka Kikosi cha Polisi wa Utalii Kenya walipelekwa Laikipia kuwalinda wageni na kambi na hoteli ambako wanako fikia.

“Kutokana na hali mbaya ya ukame, baadhi ya wafugaji wamevunja sheria kwa kuvamia maeneo ya ranchi binafsi na uhifadhi wa mazingira wakilisha mifugo iliyosababisha migogoro na wamiliki binafsi wa ardhi hizo.

Operesheni za Ulinzi

“Ni kinyume cha sheria kwa wafugaji kuvamia ardhi za watu binafsi. Polisi wameongeza ulinzi ili kuwalinda wawekezaji, wageni na mali zao,” amesema.

Akizungumza kwa simu na gazeti la the Nation Jumatatu, Owino amesema Mkuu wa Jeshi la Polisi Joseph alitembelea Laikipia Jumamosi ilikuhakikisha namna operesheni za ulinzi zinavyoendelea.

Amesema kiongozi huyo wa polisi amesisitiza nia ya dhati ya serikali katika kulinda mali na maisha ya wakazi na wageni.

Mwezi mmoja uliopita, wafugaji walivamia katika hifadhi ya Suiyan wakiwa na mifugo yao wakitafuta malisho ambapo waliunguza hoteli na nyumba ndogo za malazi.

Ranchi nyingine na maeneo ya uhifadhi wa mazingira ambayo yamevamiwa na wafugaji ni pamoja na Laikipia Nature Conservation, Segera ranch, O1 Jogi, O1 Malo Sabuk, Borana na Mpala.

Ranchi hizo na maeneo ya uhifadhi wa mazingira ndani ya kaunti ya Laikipia ni kati ya vituo vikubwa vya utalii nchini vinavyo wavutia wengi wanaopenda wanyama pori.

XS
SM
MD
LG