Tamasha hizo za siku nne, ambazo zilianza Ijumaa na kwendelea hadi Jumatatu, zilifanyika katika kituo cha utamaduni wa Wakenya waishio nje ya nchi, Kenyan Cultural Center (KCC) kilicho chini ya usimamizi wa kanisa la Kenyan American Community Church (KACC).
Sanaa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na muziki kutoka jamii tofauti za Kenya, vinyago na vyakula vya kila aina, ni baadhi tu ya vivutio vingi vilivyoleta tabasamu kwa wengi waliohudhuria.
Balozi wa Kenya kuhusu utalii na utamaduni, Emmy Kosgei, aliiambia Sauti ya Amerika kwamba maonyesho hayo ni njia mojawapo ya juhudi za kuimarisha taswira ya Kenya katika mataifa ya nje.
"Kuna mgawanyiko mkubwa uliojidhihirisha baina ya Wakenya hususan kufuatia kipindi kirefu cha uchaguzi mkuu wa mwaka jana na kupelekea sifa mbaya ya nchi hiyo hata kwa mataifa ya nje," alisema Kosgei, ambaye pia ni msanii.
"Tunataka kuonyesha ulimwengu kwamba licha ya kuwa na tofauti, Kenya ingali nchi moja na kwamba tamaduni zetu tofauti hazimaanishi kwamba tumetengana kama taifa," aliongeza.
Baadhi ya Wamarekani wanaonuia kutembelea Kenya walionekana wakiuliza maswali kuhusu hali ya maisha, jamii na vivutio mbalimbali vya kitalii katika nchi hiyo huku wakionja vyakula tofauti tofauti vya kiasili.
Wakenya waishio katika miji mabalimbali ya Marekani walileta familia zao kwa tamasha hizo.
"Ni njia nzuri ya kuwafunza watoto wetu waliozaliwa hapa Marekani kwamba tuko na mizizi dhabiti ya kitamaduni," alisema Chege Maina, mmoja wa waliohudhuria.
Mkuu wa taasisi ya KCC, Rev Dr George Gitahi alielezea kuridhishwa kwake na jinsi wageni walijitokeza kwa wingi kwa maonyesho ya mwaka huu.
"Haya ni makala ya kumi na mbili tangu tuanze maonyesho haya. Yamekuwa kivutio kikubwa na wageni wanajifunza kwamba Afrika ina mazuri na siyo tu njaa, magonjwa na vita vya kikabila," alisema.
Timothy Ndegwa, mmoja wa waandalizi wa maonyesho hayo, aliiambia Sauti ya Amerika kwamba kupitia tamasha kama hizo, Wakenya wanaoishi Marekani wanatoa ujumbe kwa wenzao kwamba ukabila unaoeneza chuki unaweza kulisambaratisha taifa.
"Tunakusudia kupanua tamasha hizi katika siku za usoni kwa sababu ya wingi wa watu wanaohudhuria," alisema Ndegwa.
Naibu gavana wa kaunti ya Nakuru, Dkt Eric Korir, alisifu maonyesho hayo na kueleza matumaini yake kwamba serikali za kaunti zitajifunza mengi na kupelekea ushirikiano mkubwa hata zaidi na Wakenya waishio nje ya nchi.
"Nimeshuhudia nidhamu ya kipekee kwa vijana wa hapa ambayo inahitaji kuigwa kule kwetu nyumbani," alisema Korir.
Kundi la Wilaya ya Smyrna lilipata tuzo la densi bora zaidi huku kikundi cha wilaya ya Catersville kikipata nafasi ya pili kwa densi yao iliyoshangiliwa sana na waliohudhuria maonyesho hayo.