Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 20:20

Hali ya utalii shwari nchini Kenya


Meli ya Marekani iliyobeba watalii yazuru bandari ya Mombasa
Meli ya Marekani iliyobeba watalii yazuru bandari ya Mombasa

Wakati Kenya ikikabiliwa na changamoto kubwa ya kupambana na mashambulizi ya kigaidi, juhudi za serikali katika kuboresha hali ya usalama nchini zimeanza kuzaa matunda.

Nchi hiyo ya Afrika Mashariki, yenye vivutio vya utalii kwenye sehemu kubwa ya ukanda wa pwani ya bahari ya Hindi tayari imeanza kupokea watalii kwa idadi kubwa ikitafsiri kuongezeka pato lake la taifa.

Kwa mujibu wa mwandishi wa idhaa ya Kiswahili ya VOA, Salma Muhamed,meli ya kwanza iliyobeba watalii ilizuru taifa hilo la Afrika Mashariki mwaka huu wa 2017.

Meli hiyo, inayojulikana kama MV Nautica iliyokuwa imefanya safari yake ikitokea Marekani iliwasili katika bandari ya Mombasa Alhamisi ikiwa na jumla ya watalii 1, 049.

Watalii hao wakiwemo wanaume na wanawake wamepanda meli hiyo kutoka Florida, Marekani na safari yao iliwachukua miezi sita.

Kwa mujibu wa mwandishi wetu watalii hao ni raia kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Marekani, Uingereza, Canada, na Denmark.

Meli hiyo iliwasili bandarini majira ya asubuhi ikiwa imetokea Zanzibar, kabla ya kuendelea na safari yake kwenda mjini Victoria nchini Ushelisheli. Kwa ujumla meli hii ambayo ni kubwa imekuwa katika ziara ya kitalii katika nchi mbalimbali zilizoko katika bahari ya Hindi.

Watalii wengi hupenda kutembelea nchi za Afrika Mashariki zilizoko katika ukanda wa bahari kutokana na maji yake masafi na tulivu. Upepo wake ni mwanana na wakati mwingi haina dhoruba

Kihistoria, hii ni mara ya pili kwa MV Nautica kuwasili Kenya, baada ya kuzuru bandari hiyo ya Mombasa. Huu ni mfululizo wa juhudi ya Serikali ya Kenya katika kuimarisha biashara ya Utalii nchini.

Bandari ya Mombasa ndio kubwa zaidi kanda ya Afrika Mashariki na Kati, na imekuwa na mchango mkubwa hasa kwa mataifa yasiyopakana na bahari kama vile Uganda, Rwanda na Burundi.

Kabla ya kuondoka mjini Mombasa watalii hao walipata fursa ya kutembelea na kujionea wenyewe maeneo muhimu ya kihistoria ikiwemo ngome maarufu ya Fort Jesus iliyojengwa na Ureno kati ya mwaka wa 1593 na 1596.

Hatua ya meli hiyo maarufu ya kitalii kuzuru nchi Kenya imeonekana kuongeza imani kwa watalii na inathibitisha kuwa sekta ya utalii inaendelea.

Pamoja na tahadhari iliyotolewa na mataifa ya Ulaya ikiwataarifu watalii wa kigeni kutozuru pwani ya Kenya kutokana na sababu za kiusalama, juhudi za serikali zimeonyesha kurejesha imani ya watalii wengi, katika nchi mbalimbali duniani.

Mnamo mwaka jana 2016 pia meli nyingine ya kitalii ya MS Silver ilitia nanga katika bandari hiyo ya Mombasa.

Hii inakuja wakati ambapo bodi ya utalii nchini Kenya (KTB) ikiendelea na harakati za kutangaza utalii wa taifa hilo kimataifa, na kukanusha uvumi kuwa kuna uvunjifu wa amani na tishio la kigaidi.

Akizungumza na wanahabari bandarini humo afisa wa mawasiliano wa mamlaka ya bandari nchini Kenya (KPA), Hajji Masemo amesema kuwa wameanza rasmi ujenzi wa sehemu ya kisasa ya kupokea meli za kitalii.

“Tunatarajia kuwa na sehemu ya kisasa ya kupokea meli ifikiapo mwanzo wa msimu mwingine wa kitalii mwezi Septemba mwaka huu,” alisema Masemo.

Ujenzi huo utaigharimu KPA shilingi milioni 150, sawa na dola milioni 1.5 za Kimarekani.

Kampuni ya Trade Mark East Afrika nayo imeahidi kuchangia dola milioni 1 katika ujenzi huo.

Wakati juhudi za serikali zikiendelea kuhakikisha usalama wa watalii hilo ni kipaumbele cha taifa hasa ikizingatiwa kuwa utalii unachangia uchumi wa Kenya kwa kiwango kikubwa.

KTB inasema: “Tunatarajia meli nyingi zaidi za kitalii kutia nanga Mombasa mwaka huu”.

Imeandaliwa na mwandishi wetu Salma Muhamed, Kenya





XS
SM
MD
LG