Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 21, 2024 Local time: 17:30

Utalii, michezo vyaboresha maisha wilaya ya Gulu Uganda


Wilaya ya Gulu, Uganda
Wilaya ya Gulu, Uganda

Kwa muda mrefu, wilaya ya Gulu iliyo kaskazini mwa Uganda imekuwa na sifa mbaya kutokana na migogoro ya kisiasa tangu wakati wa utawala wa rais Milton Obote, aliyeongoza Uganda mara mbili hadi mwaka wa 1985.

Vita baina ya waasi wa kundi la LRA lililoongozwa na Joseph Kony na majeshi ya taifa ni mambo yaliyo dhoofisha ustawi wa wilaya ya Gulu na maeneo mengine ya nchi hiyo, hadi pale vita vilipomalizika takriban miaka mitano iliyopita.

Lakini sasa mji wa Gulu unaendelea kuvuta taswira mpya na kusuhudia mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na kuboresha sekta ya utalii – zaidi kwa kuwapokea wageni kutoka nchi mbali mbali za bara la Afrika.

Mwezi huu wa Agosti Gulu imepokea idadi kubwa ya wageni, ambao wengi ni maelfu ya vijana kutoka nchi zote za Afrika Mashariki, wanaoshiriki michezo ya kila mwaka baina ya shule za sekondari eneo zima la Afrika Mashariki.

Kuanzia juma lililopita wanamichezo chipikizi kutoka shule zaidi ya 200 za Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi waliwasili katika mji wa Gulu ili kushindana katika aina ya michezo 13 hadi mwishoni mwa mwezi huu.

Hii ni ishara nzuri katika juhudi za kuijenga upya Gulu na kuhakikisha maelfu ya wenyeji wa wilaya hiyo iliyo na raia karibia 200,000, watanufaika na kuweka matumaini ya maisha licha ya vita vilivyowatatiza miaka ya nyuma.

Mnamo Machi mwaka huu Manispaa ya Gulu iliteuliwa kuandaa michezo hiyo muhimu kanda ya Afrika Mashariki – na uwanja mkuu unaotumika unapatikana katika chuo cha Mtakatifu Joseph Layibi.

Ushindani baina ya wanamichezo hao chipukizi pamoja na wakufunzi na mamia ya waalimu wanaoshirikishwa, pia ni njia moja ya kuboresha uhusiano katika Jumuia ya Afrika Mashariki.

Michezo inayotarajiwa kuwa na mvuto na ushindani mkubwa ni pamoja na kandanda, riadha, rugby, na mpira wa kikapu.

Wenyeji Uganda wana rekodi nzuri ya kushinda taji la kandanda tangu michezo hiyo ilipozinduliwa miaka 15 iliyopita, wakati Tanzania ikijiandaa kupambana na Kenya katika ubingwa wa mbio za masafa marefu.

Vijana wa Rwanda wameapa mwaka huu kuvua Kenya matawi ya mpira wa kikapu, japo Kenya imekuwa ikifanikiwa kila mwaka kutwaa ubingwa huo.

Kushindana uwanjani na kujenga uhusiana katika eneo la Afrika Mashariki sio mwisho wa michezo hiyo – manufaa zaidi ni masomo ya vyuo vikuu na ajira ambazo vijana wanapata kutokana na vipawa na uhodari wa kucheza.

Kocha Mkenya Philip Onyango ambaye hadi sasa ameshinda mataji mengi zaidi eneo la Afrika Mashariki, ameiambia idhaa ya Kiswahili VOA kuwa anajivunia kwa kuongoza shule mbali mbali kusinda ubingwa wa mpira wa kikapu.

Baadhi ya wachezaji waliopitia mikononi mwa kocha Onyango walifanikiwa kusomea vyuo tofauti huko Marekani na hata kufanya kazi katika majimbo mbali mbali ya Marekani.

Kocha huyo anayejichukulia kama mzazi wa vijana wengi anaamini kuwa hilo linazidi kumpa nguvu za kuendelea kunawiri, na kuwa kocha bora zaidi wa vijana hata katika bara la Afrika.

Maelfu ya watu kutoka maeneo mbali mbali nchini Uganda wamesafiri katika wilaya ya Gulu iliyo kilomita 350 kutoka mji mkuu wa Kampala, ili kushuhudia michezo hiyo inayotajwa kama ya kusisimua.

Imetayarishwa Mwandishi wetu, Josephat Kioko, Uganda

XS
SM
MD
LG